Mtumishi wa TRA kortini madai ya kupokea rushwa

28Sep 2020
Jumbe Ismaily
Nzega
Nipashe
Mtumishi wa TRA kortini madai ya kupokea rushwa

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Wilaya ya Nzega, mkoani Tabora imempandisha kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mfawidhi mtumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wa wilaya hiyo, Dickson Mtandu Mtandu, kwa tuhuma za kuomba rushwa ya Sh. milioni 1.5 kutoka kwa mfanyabiashara ..

wa nyumba ya kulala wageni.

Mwendesha Mashtaka wa TAKUKURU Wilaya ya Nzega, Mazengo Joseph, alidai, kwamba mtuhumiwa alitenda kosa hilo kinyume cha Kifungu cha 15 (1) (a)(2) na 3(a) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na.11/2007.

Mwendesha mashtaka huyo alidai mbele ya Hakimu wa Wilaya ya Nzega, Joseph Mwita, kwamba kati ya Agosti 26, mwaka huu na Agosti 28, mwaka huu kwa nyakati tofauti mshtakiwa akiwa eneo la Mery Pud mjini Nzega, aliomba rushwa ya Sh. 1,500,000 kutoka kwa Sahani Katuli ili asimchukulie hatua za kisheria kwa kutotoa risiti ya EFD katika nyumba yake ya kulala wageni ya Kipozo ilioko mjini Nzega.

Aidha, Mazengo alidai pia kwamba Agosti 29, mwaka huu, mshtakiwa alikamatwa na maofisa wa TAKUKURU Wilaya ya Nzega wakati akipokea rushwa ya Sh. 400,000 kati ya Sh. 1,500,000 alizokuwa ameomba kutoka kwa mlalamikaji baada ya kuwekewa mtego na taasisi hiyo.

Hata hivyo, mshtakiwa huyo baada ya kusomewa shtaka, alikana kutenda kosa hilo, na yupo nje kwa dhamana ya shilingi milioni moja na wadhamini wawili hadi Oktota 20, mwaka huu itakapotajwa.

Habari Kubwa