Mtwara waadhimisha sherehe za Idd kwa kuchangia damu

21Jul 2021
Abdallah Khamis
MTWARA
Nipashe
Mtwara waadhimisha sherehe za Idd kwa kuchangia damu

WAUMINI wa dini ya Kiislam katika Manispaa ya Mtwara Mikindani, mkoani Mtwara, wamesherehekea Sikukuu ya Eid al-Adha kwa kujitolea uchangiaji wa damu kwa ajili ya kuwasaidia wagonjwa katika hospitali mbalimbali mkoani humo.

Uchangiaji huo umefanyika katika viwanja vya saba saba mkoani humo, baada ya kumalizika ibada ya swala ya Eid al-Adha na kufuatiwa na hotuba iliyosomwa na Idrisa Bakari, ambaye ni  Imamu  wa Masjid Noor,

Katika hotuba yake ya Imamu Bakari amewaasa waislamu na Watanzania kwa ujumla kuishi kwa wema na kuwasaidia wasiojiweza, huku wakihakikisha wanakuwa chanzo cha kulinda amani isivurugike.

Amesema uislamu unatambulika kwa matendo ya wema yanayofanywa na waumini wa dini hiyo, ikiwa ni pamoja na kuwasaidia wagonjwa na wasiojiweza, hivyo ni wajibu wa waumini kuhakikisha utambulisho huo haupotei.

Katika hatua nyingine Imamu Bakari amewaomba viongozi wa serikali kuzuia sherehe zenye kusababisha usumbufu na kelele kwa watu na kuzitaja sherehe hizo kuwa ni zile zinazovunja maadili ya Kitanzania.

Amesema kwa sasa kumezuka tabia ya watu kukesha zaidi ya siku tatu kwenye maeneo ya mikusanyiko ya watu kwa madai ya kujiandaa na sherehe wanazotarajia kufanya baadae.

"Hii tabia ya watu wana sherehe jumapili lakini wanaanza kuzunguka mitaani kuanzia Ijumaa mizunguko hii wakati mwingine inapoteza hata heshma ya wahusika tunaomba serikali izuie kwa ajili ya kulinda maadili yetu watanzania” amesema Imam Bakari