Mufti atafsiri tetemeko Bukoba, kupatwa kwa jua

13Sep 2016
Elizaberth Zaya
Nipashe
Mufti atafsiri tetemeko Bukoba, kupatwa kwa jua

MUFTI Mkuu wa Tanzania, Sheikh Abubakari Zuberi, amesema matukio ya kupatwa kwa jua na tetemeko la ardhi yaliyotokea nchini ndani ya siku 10 kati ya Septemba mosi na Septemba 10, ni ishara ya Mwenyezi Mungu kuwakumbusha watu wake kutafakari mahali walipokosea na kumrudia.

Akizungumza katika Swala ya Eid El-Haji ambayo kitaifa ilifanyika Makao Makuu ya Baraza Kuu la Waislam Tanzania (Bakwata), Kinondoni Jijini Dar es Salaam, Mufti Mkuu alisema matukio hayo hayawezi kutokea hivi hivi isipokuwa Mola kuwakumbusha watu wake kumrudia.

Kutokana na hali hiyo alisema watu wanapaswa kurudi katika nyumba za ibada, kumuomba Mungu awaepushie mambo mabaya wao na nchi kwa ujumla.

“Mtume alisema jua na mwezi ni ishara mbili za kuzibua kudra za Mwenyezi mungu, yaani kuleta mema, hivyo hawezi kuvifanya vipatwe isipokuwa inapotokea hivyo ni ishara ya kuwataka watu wake wamrudie," alisema Sheikh Zuberi.

"Lakini badala ya watu kukimbilia katika nyumba za ibada kumuomba aepushe balaa lipite wanalifanya ni jambo la kutalii!

“Vivyo hivyo tetemeko la ardhi nalo ni ishara ya Mwenyezi Mungu kutaka watu wake wamrudie.

"Ninawapa pole watu waliokumbwa na tatizo hilo na wale waliopoteza ndugu zao kupitia tukio hilo, ila ni vema watu wote tukakimbilia katika nyumba za ibada na kumuomba (Mungu) atuondoshee matatizo katika nchi, lakini eti watu wanatalii, Mwenyezi mungu anatalihiwa?”

KURUBUNIWA
Sheikh Zuberi pia aliwataka Watanzania kuwa wazalendo na nchi yao na kuepuka kurubuniwa na mtu yeyote kuvuruga amani ya nchi.

Alisema wananchi ni vema wakajifunza mema na tabia njema katika kueneza maadili, wenye kutenda haki na kushikamana na kwamba endapo watafanya hivyo wataepuka watu wasio na nia njema na nchi yao; wenye nia ya kuvuruga amani iliyopo.

“Ukijitambua na kujua wewe ni Mtanzania na wajibu wako katika nchi huwezi kukubali kurubuniwa na mtu mmoja kutoka ndani au nje akakushawishi kuiharibu amani," alisema Mufti Mkuu.

"Unatakiwa pia kutafuta uchumi kwa ajili yako na nchi yako, una umuhimu wa kuona nchi yako haiingiliwi kwa nia ovu na mtu yeyote, unatakiwa wewe mwenyewe uwe ni mchumi, unakuwa mwenyewe ndiye mwenye nchi lakini pia mlinzi, na ukijitambua hivyo huwezi kushawishiwa kuiharibu wakati ndugu zako wote katika nchi hiyo ukaleta uharibifu, labda uwe huna uchungu na hujitambui.”

Alisema Watanzania wanahitaji kuvumialiana hata pale wanaopoona wamefanyiwa jambo baya na kwamba kufanya hivyo kutaendelea kuiweka nchi katika hali nzuri na ya amani.

Aidha, Sheikh Zuberi alisema katika kipindi hiki ambacho serikali ya awamu ya tano inajenga nchi yenye viwanda, ipo haja kwa kila mmoja kuunga mkono azma hiyo kwa kufanya kazi kwa bidii.

Alisema zipo fursa nyingi ambazo Watanzania wanaweza kufanya na kulisaidia taifa kusonga mbele ikiwamo katika sekta ya kilimo.

Mbali na hilo pia aliwataka kufanya kazi kulingana na taaluma zao na kupendelea kujifunza masuala mbalimbali ya kidini na kidunia katika kufanikisha malengo yao na ya nchi.

Alisema serikali pekee haiwezi kufanikisha kufikia malengo, lakini endapo kila mtu atashiriki itakuwa ni rahisi kuyafikia malengo hayo.

Sheikh Zuberi alisema Bakatwa ina mpango wa kufungua vyuo katika kila mkoa kwa ajili ya kuelimisha waislam na kuandaa watu ambao watakuwa viongozi, na kwamba watakuwa wanafundishwa masuala ya dini na masuala mengine ya utawala na namna ya kuishi.

Habari Kubwa