Muhimbili yaanza kuondoa uvimbe bila upasuaji

15Jun 2019
Beatrice Shayo
DAR
Nipashe
Muhimbili yaanza kuondoa uvimbe bila upasuaji

HOSPITALI ya Taifa ya Muhimbili (MNH), imeanza kufanya matibabu ya kuondoa uvimbe kwenye kizazi (Uterine fibroids) bila kufanya upasuaji.

Daktari Bingwa wa Tiba Radiolojia wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dkt. Flora Lwakatare akizungumza na waandishi.

Hayo yalisemwa jana jijini Dar es Salaam na Daktari Bingwa wa Radiolojia, Flora Lwakatare, wakati akizungumza na waandishi wa habari.

Alisema MNH kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Yale na vyuo shiriki vya Emory na Dartmouth vya nchini Marekani, ilianzisha programu maalum ya mafunzo ya tiba  ya radiolojia tangu mwaka 2008.

"Tumeweza kutibu uvimbe kwenye kizazi kwa mgonjwa mmoja kupitia tiba ya radiolojia kwa kuingiza mpira wenye chembechembe maalum kwenye mishipa ya damu ambazo zinakwenda kuziba mishipa hiyo inayopeleka damu kwenye uvimbe," alisema.

Dk. Lwakatare alisema baada ya mishipa kuziba, uvimbe unakosa damu au chakula chake na kuanza kusinyaa na kufa.

Alisema mama mwenye uvimbe kwenye kizazi hakuna haja ya kumfanyia upasuaji mkubwa.

Dk. Lwakatare alisema tatizo hilo ni kubwa kwa kuwa kati ya wanawake 10 wanaopimwa wanne wanakutwa na ugonjwa huo.

"Hatari kubwa kama una huo uvimbe utakusababishia kutoweza kupata mtoto, kupoteza damu kwa wingi na hata kupata maumivu makubwa. Kinamama wengi wanatembea nao, madhara ya uvimbe unapokua unasababisha kukosa uzazi, lakini kwa tiba hii tunayoitoa utapata mtoto," alisema.

Aidha, alisema wakufunzi wa awamu ya nne tangu ushirikiano huo uanze umehusisha madaktari bingwa, mafundi sanifu radiolojia, wauguzi wa radiolojia kutoka chuo Kikuu cha Emory na Yale Marekani pamoja na hospitali iliyopo Buffalo, New York, wakiongozwa na Dk. Janice Newsome.

Alisema katika awamu hiyo huduma ambazo zimetolewa ni utoaji wa sampuli kutoka kwenye uvimbe sehemu mbalimbali za mwili ambazo si rahisi kufikiwa bila upasuaji mkubwa.

Dk. Lwakatare alisema walizibua mirija ya nyonga, kuweka mirija kwenye figo, mirija ya mkojo iliyoziba na unyonyaji wa uvimbe wenye maji na usaha ikiwa ni mwendelezo wa huduma hiyo.

Alisema tiba hiyo inafaida inawezesha kuepuka upasuaji mkubwa ambao una vihatarishi, kuepuka kukaa hospitali kwa muda mrefu kwa kuwa wanaofanyiwa tiba hiyo ya radiolojia mara nyingi hurudi nyumbani siku hiyo hiyo.

"Hii tiba inapunguza gharama kwa mgonjwa maana ukishapatiwa matibabu unaondoka siku hiyo hiyo sio kwamba utalazwa," alisema.

Alisema kipindi cha nyuma tiba hizo huwa zinahitaji upasuaji mkubwa na kulazwa hospitalini kwa muda mrefu.

Aidha, alisema tangu waanzishe huduma hiyo wagonjwa 339 wamepatiwa huduma ya kibingwa ya tiba radiolojia wengi wakiwa wagonjwa wenye uvimbe kinywani.

Alisema wagonjwa wenye uvimbe wa kinywa walikuwa wakipelekwa nchini India kutibiwa kwa gharama ya Sh. milioni 99, kwa sasa Hospitali ya Muhimbili wanaitoa kwa Sh. milioni mbili.

Aidha, alisema wamepatiwa ujuzi mpya wa kuweka mipira maalum kwenye mishipa mikubwa ya damu ambayo itawanufaisha wagonjwa wa figo walio kwenye mfumo wa kusafisha damu au wanaopatiwa tiba ya saratani.

Dk. Newsome alisema wamekuja kubadilishana uzoefu na madaktari wa Tanzania na suala la muhimu ni kushirikiana ili kutekeleza majukumu yao.

 

Habari Kubwa