Muhimbili yanunua mashine mbili za kupandikiza uloto

10Sep 2021
Mary Geofrey
DAR ES SALAAM
Nipashe
Muhimbili yanunua mashine mbili za kupandikiza uloto

HOSPITALI ya Taifa Muhimbili (MNH) imenunua mashine mbili maalum aina ya Spectra Optia, zenye thamani ya Sh. milioni 245 zitakazosaidia kutoa tiba ya magonjwa 10 ikiwamo huduma ya upandikizaji uloto.

Mashine hizo zitasaidia kuvuna chembechembe mama za kuzalisha damu (haematopoietic stem cells), mazao ya damu ikiwamo chembe sahani (Platelets), chembe nyeupe (granulocytes) na  Utegili (Plasma).

Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Damu na Mkuu wa Kitengo cha Magonjwa ya Damu wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Stella Rwezaula, anatambulisha huduma hiyo mpya kuwapo nchini katika hospitali hiyo leo Jijini Dar es Salaam.

Anasema huduma hiyo, inasaidia kupunguza idadi ya wachangiaji wa damu kwa mgonjwa mmoja kutoka sita hadi 12 na kuwa mchangaji mmoja.

Aidha, mashine hizo zinamsaidia mchangiaji kuchangia tena baada ya wiki mbili, tofauti na mfumo wa zamani wa uchangiaji ulilazimu kuchangia tena baada ya miezi mitatu hadi minne.