Muhimbili kutoa huduma ya kujifukiza  

25Feb 2021
Yasmine Protace
Dar es Salaam
Nipashe
Muhimbili kutoa huduma ya kujifukiza  

HOSPITALI ya Taifa Muhimbili (MNH), imesema kwa kutambua umuhimu wa tiba asili,  itafunga mashine za kujifukiza kwa ajili ya wagonjwa ambao wamekuwa wakihitaji huduma hiyo wanapokuwa wakipatiwa huduma za kibingwa.

Hayo yalibainishwa jana na Mkuu wa Kitengo cha Habari na Uhusianowa Hospitali hiyo, Aminieli Aligaesha, kwamba hospitali itaweka  sifa na viwango gani vya mtu kuingia kwenye mashine hiyo kwa kuwa huduma hiyo itakuwa kama nyongeza katika kuwahudumia wananchi wanaofika kupata huduma.

Alisema hayo jijini Dar es Salaam wakati wa ziara ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Dorothy Gwajima, ya kuwatembelea  wazalishaji wa bidhaa za tiba asili.

Wazalishaji hao ni NIMRCAF, Uzima Herbar Drops, FUKIZA UDANOL, Bingwa Mix spices na Bupil za jijini Dar es Salaam.

Aligaesha alisema hospitali hiyo, imenunua mashine nne ambazo tatu zitafungwa kwenye tawi la Upanga na moja kwenye Mloganzila, na kwamba zinatarajiwa kufungwa mwishoni mwa wiki hii.

Baada ya kuwatembeleza wazalishaji hao, Waziri Gwajima alisema bidhaa  zote zinazotengenezwa na wataalamu wa  tiba asili lengo lake ni nchi kuwa na njia mbadala  kwa njia yoyote.

“Tiba asili ilikuwapo tangu muda mrefu toka miaka ya 1990, na ilishaandikwa  kwenye maandiko ya wizara pamoja na Sera ya Afya ya Mwaka 2007, hivyo bidhaa zote zilizotengenezwa na wataalamu wa tiba asili lengo ni kuwa na nia ya kuitafuta tiba kama nchi kwa njia yoyote,” alisema.

Dk. Gwajima alisema umefika wakati sasa wa kuzalisha kwa pamoja ili kuitendea haki Ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kuwa na viwanda na kufanya utafiti kwa kuinua bidhaa za tiba asili.

“Lazima tuhitaji mkono wa vyuo vikuu ili kwenda kama timu badala ya kubeba suala la nchi kama la wizara moja, nyinyi UDSM (Chuo Kikuu cha Dar es Salaam) mnashirikiana vipi na China?” Alihoji.

“Lazima tuwe na kamati ambayo itatufanya tukimbie haraka ili kuwa na jukumu la pamoja la tiba asili katika kuzuia magonjwa ya kuambukiza na yasiyoambukiza ili tuweze kufikia faida za kiafya na za kiuchumi.”

Aliongeza kuwa, changamoto ya kupumua zinawapata watu wengi, hivyo inatakiwa kuwafika wananchi wote na kwa rika zote kuanzia watoto wa shule ya msingi, na watoto wajengewe mazoea na uelewa kwamba lishe bora ni ipi na msingi wake uanzie toka utotoni.

“Ninawatambua wazalishaji wote wa tiba asili na watoa huduma, ambao wamesajiliwa na Baraza la Tiba Asili/Mbadala, tutaendelea kuwatembelea wote kisha tutakuja na kikao cha kujumuisha mafanikio na changamoto zote pamoja na vyuo vyetu vikuu ambavyo vinafanya utafiti na taasisi zetu ili tuwe na njia ya kwenda mbele na kwa haraka pamoja,” alisema.

Aliwapongeza wazalishaji wote wa tiba asili, na kuahidi serikali inawaunga mkono kwa juhudi wanazofanya, hivyo itasaidia kuleta mapinduzi ya tiba asili nchini.

Naye Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Prof. William Anangisye, alisema chuo chake kipo tayari kusaidia utafiti mbalimbali ili kuwe na matokeo chanya kwani wao wanamilikiwa na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hivyo matarajio yao ni kuongeza thamani ya tiba asili.

Habari Kubwa