Muhimbili yafanya upasuaji uvimbe kwenye ubongo

19Jun 2019
Beatrice Shayo
Dar es Salaam
Nipashe
Muhimbili yafanya upasuaji uvimbe kwenye ubongo

HOSPITALI ya Taifa ya Muhimbili-Mloganzila kwa mara ya kwanza imeanza kufanya upasuaji mkubwa wa kuondoa vivimbe katika mishipa ya damu kwenye ubongo.

Upasuaji huo ambao umechukua muda wa takribani saa sita umefanywa na wataalamu wa Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila kwa kushirikiana na daktari bingwa mshauri wa upasuaji wa ubongo na mishipa ya fahamu, Profesa Hun Seong, kutoka Yonsei, Korea Kusini.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, daktari bingwa wa upasuaji wa ubongo na mishipa ya fahamu katika Hospitali ya Muhimbili-Mloganzila, Dk. Raymond Makundi, alisema wamefanya upasuaji huo kwa mgonjwa mmoja ambaye kwa sasa anaendelea vizuri na ataruhusiwa kuondoka.

Alisema wagonjwa waliokuwa wanahitaji huduma hiyo walikuwa wanapelekwa nje ya nchi kwa ajili ya kupatiwa matibabu ambayo iliwagharimu fedha nyingi.

Alisema kutokana na uchache wa wataalamu na ukosefu wa vifaa tiba hivyo, mgonjwa kama huyo angepelekwa nje ya nchi angelipia Sh. milioni 40.

Aidha, alisema tatizo la vivimbe katika mishipa ya damu kwenye ubongo hutokana na sababu mbalimbali ikiwamo kurithi vinasaba ambayo mtu huzaliwa navyo, uvutaji wa sigara, na maambukizi ya vijidudu kama bakteria vinavyoathiri mishipa ya damu.

Dk. Makundi alisema ugonjwa huo huchelewa kugundulika kutokana na watu kutokufahamu dalili za hatari za ugonjwa huo na upungufu wa vifaa vya uchunguzi pamoja na wataalamu wa kulibaini tatizo hilo mapema.

“Baadhi ya dalili ni kupata maumivu makali ya kichwa, kuona vitu viwili viwili na kupoteza fahamu,” alisema.

Dk. Makundi alisema vishipa vinapopasuka wagonjwa wanafika hospitali wakiwa na ugonjwa wa kiharusi, hivyo wanatibiwa kama wana viharusi kutokana na kukosa uelewa.

Makunda alisema ugonjwa huo huwaathiri wenye umri kuanzia miaka 30 hadi 60 na hospitali hupokea wagonjwa kati ya wanne hadi sita kwa mwezi.

Naye daktari wa upasuaji wa ubongo na mishipa ya fahamu, Dk. Alvin Miranda, akielezea upasuji huo, alisema lengo la upasuaji ni kufunga vivimbe hivyo kwa kutumia vifaa tiba maalum (aneurysm clips) ili kuzuia damu isiendelee kuvuja katika ubongo.

“Mgonjwa anapopata tatizo la kuvuja damu kwenye ubongo kwa mara ya kwanza anakuwa katika hatari ya kupoteza maisha kwa asilimia 30, wakati akivuja damu kwa mara ya pili inaweza kusababisha kifo kwa asilimia 70 hadi 80,” alisema Dk. Miranda.

Alisema kitakwimu wastani wa asilimia tatu ya watu duniani hupata tatizo hilo kila mwaka na nusu yao ambao huwahi kufika hospitalini mishipa inapopasuka huku wengine wakipoteza maisha kabla ya kufikia huduma.

Dk. Miranda alisema asilimia 50 ya wagonjwa hufika hospitali na asilimia 50 hutibiwa kwa tiba ya kiharusi.

Naibu Mkurugenzi wa hospitali hiyo, Dk. Julieth Magandi, alisema wamefurahi kwa kuanza upasuaji huo na utasaidia kupunguza gharama za rufani za nje ya nchi.