Muhimbili yapokea vifaa vya mil. 300/- kutoka Korea

10Aug 2020
Mary Geofrey
Dar es Salaam
Nipashe
Muhimbili yapokea vifaa vya mil. 300/- kutoka Korea

HOSPITALI ya Taifa Muhimbili (MNH)- Mloganzila imepokea msaada wa vifaa tiba wenye thamani ya Sh. milioni 335 kutoka kwa taasisi inayojihusisha na masuala ya afya ya Korea Kusini (KOFIH).

Mkurugenzi Mkuu wa MNH, Prof. Lawrence Museru, akipokea msaada huo mwishoni mwa wiki, alisema hospitali hiyo imekuwa na ushirikiano na taasisi hiyo tangu mwaka 2017.

"Ushirikiano uliopo kwa sasa kati ya taasisi hizi mbili ni kujenga uwezo kwa Hospitali ya Mloganzila katika maeneo makuu mawili ambayo ni mafunzo na vifaa tiba. Leo hii tumekabidhiwa vifaa ikijumuisha vya kufanyia upasuaji vilivyogharimu Sh. milioni 96 na vya ufundi kwa ajili ya matengenezo ya vifaa tiba vyenye gharama ya Sh. milioni 235," alisema Prof. Museru.

Alisema vifaa hivyo vitasaidia kuongeza nguvu katika upasuaji wa masikio, pua na koo katika hospitali hiyo.

Alitaja aina ya vifaa hivyo kuwa ni vya kufanyia upasuaji wa mafindofindo na nyama za pua (Tonsillectomy and Adenoidectomy) seti sita, vifaa vya uchunguzi wa masikio, pia na koo (Basic ENT) seti mbili, vifaa vya kufanyia upasuaji wa masikio na upandikizaji wa vifaa vya usikivu masikio (Mastoideoctomy), seti nne.

Vingine ni vifaa vya upasuaji wa koo kwenye njia ya hewa (Tracheostomy), seti tatu na vifaa vingine.

Prof. Museru, alisema pia wanashirikiana kuwapatia mafunzo wataalamu wa afya katika idara mbalimbali.

"Taasisi hii pia imetusaidia kutoa mafunzo kwa wataalamu wa afya tumepata madaktari bingwa kutoka katika vyuo mbalimbali vya Korea Kusini na hata sasa tunao madaktari wao wanaowajengea uwezo madaktari wetu," alisema Prof. Museru.

Kwa upande wake, Naibu Mwakilishi Mkazi wa KOFIH Kim Jungyoon, alisema taasisi hiyo itaendelea kushirikiana na hospitali hiyo ili kuboresha huduma za afya nchini.

"Ni heshima kuwa na nafasi hii na ushirikiano mzuri kati ya KOFIH na Hospitali ya Mloganzila tutaendelea kushirikiana katika mafunzo na vifaa tiba," alisema Kim.

Habari Kubwa