Muhongo atoa mkono Idd

27Jun 2017
Sabato Kasika
Dar es salaam
Nipashe
Muhongo atoa mkono Idd

MBUNGE wa Musoma Vijijini (CCM), Prof. Sospeter Muhongo, ametoa ng’ombe watatu katika misikiti mitatu jimboni mwake kwa ajili ya sikukuu ya Idd.

Prof. Sospeter Muhongo.

Kwa mujibu wa mbunge huyo, misikiti iliyopata msaada huo ni Rukuba, Bwai Kumusoma na Busekera sambamba na kila msikiti kupata kilo 100 za mchele na lita 20 za mafuta ya kula.

“Katika kuadhimisha sikukuu ya Idd nimeungana na wenzetu Waislamu kwa kuchangia chakula katika misikiti mitatu jimboni kwangu na ninawatakia sikukuu njema na tuendelee kuchapa kazi kwa ajili ya maendeleo ya jimbo letu,” alisema Prof. Muhongo.

“Huku jimboni kwetu tuna utaratibu wa kushirikiana katika mambo mbalimbali kwa lengo la kuimarisha umoja wetu, hivyo tutaendelea kushirikiana kwa ajili ya maendeleo ya Musoma Vijijini,” alisema.

Wakati huo huo, Prof. Muhongo, ambaye ni mwenyekiti wa wabunge wa Mkoa wa Mara katika shughuli za maendeleo mkoani humo, alisema vijana 60 wamemaliza mafunzo ya kutumia umeme wa jua kwa ajili ya biashara inayotumia nishati hiyo.

Alisema mafunzo hayo yaliyoendeshwa na mtaalamu kutoka Korea Kusini, Dk. Chol, yalianza Juni 17 hadi Juni 24 yakishirikisha vijana kutoka wilayani Tarime katika majimbo ya Tarime Mjini na Tarime Vijijini.

Alifafanua kuwa mafunzo hayo ni mwendelezo wa yale ambayo yameshafanyika katika majimbo ya Musoma Vijijini, Serengeti na Bunda, huku wabunge wa mkoa huo wakiwa ni waratibu.

Habari Kubwa