Muhudumu wa baa auawa nyumba ya kulala wageni

27Oct 2016
Na Mwandishi Wetu
GEITA
Nipashe
Muhudumu wa baa auawa nyumba ya kulala wageni

MHUDUMU wa baa na nyumba ya kulala wageni, Steven Leonard (25), wilayani Geita, amekutwa ameuawa kwa kupigwa na kitu chenye ncha kali kichwani akiwa kwenye chumba chake.

Tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia jana katika nyumba hiyo, katika Mtaa wa Elimu, Kata ya Nyankumbu.

Akizungumuzia tukio hilo, mmiliki wa nyumba hiyo, Hassan Mshora, alisema taarifa ya tukio hilo aliipata jana kutoka kwa meneja wake kuwa mhudumu wake ameuawa kwa kuchinjwa.

Alisema baada ya kufika eneo hilo alikuta mhudumu huyo akiwa ameuawa na alikwenda kutoa taarifa kituo cha polisi Geita. Alisema mbali na kufanywa mauaji hayo, watu hao walipora fedha tasilimu Sh. 300,000.

“Marehemu alikuwa ni mfanyakazi wangu hapa alikuwa na muda wa mwezi mmoja anafanya kazi chumba hiki alicho fia marehemu ni cha kulala wahudumu wanaume na kutunzia mizigo yao,” alisema.

Ofisa Mtendaji wa Kata ya Nyankumbu, Agnes Lukandya, alisema taarifa za tukio hilo alizipata jana na alishuhudia mwili huo ukiwa na majeraha kichwani.

Akithibisha kuwepo kwa tukio hilo, Kamanda wa Polisi mkoani Geita, Mponjoli Mwabulambo, alisema chanzo cha mauaji hayo hakijafahamika na polisi wanaendelea na uchunguzi.

Habari Kubwa