Mume anusurika kifo baada ya kuchomwa kisu na mkewe

18Oct 2021
Marco Maduhu
SHINYANGA
Nipashe
Mume anusurika kifo baada ya kuchomwa kisu na mkewe

SIMON Robert (43) Mkazi wa Katunda Ibinzamata Manispaa ya Shinyanga, amenusurika kifo baada ya kuchomwa kisu na mkewake Amina Hamis (32), maeneo ya kichwani na tumboni, na kumsababishia majeraha.

Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga George Kyando.

Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga George Kyando, akitoa taarifa ya tukio hilo leo kwa vyombo vya habari, amesema tukio hilo limetokea  usiku wa kuamkia leo majira ya saa 7, ambapo mwaume huyo alinusurika kifo mara baada ya kuchomwa kisu na mkewake.

Amesema chanzo cha tukio hilo ni wivu wa kimapenzi, ambapo wanandoa hao walianza kugombana, mara baada ya kutoaminiana kwenye mahusiano yao, ndipo mwanamke alipochukua kisu na kumchoma mwenzake kichwani na tumboni.

“Majeruhi amelazwa katika Hospitali ya Rufani mkoani Shinyanga akipatiwa matibabu, na hali yake ni mbaya sababu alichomwa kisu sehemu mbaya za kichwani na tumboni,”amesema Kyando.

Aidha, amesema Jeshi la Polisi limamshikilia mwanamke huyo kwa tuhuma za kumchoma mume wake kisu, ambapo upelelezi ukikamilika atafikishwa mahakamani kujibu mashitaka yanayomkabili kwa mujibu wa sheria.

Katika hatua nyingine Kamanda alitoa wito kwa wanandoa wote, wajiepushe na masuala ya wivu wa kimapenzi, ambapo kama wana migogoro wakae wazungumze, na siyo kujichukulia sheria mkononi na kuanza kuchomana visu. 

Habari Kubwa