Muswada wa Habari wapita

07Nov 2016
Augusta Njoji
DODOMA
Nipashe
Muswada wa Habari wapita

MUSWADA wa Sheria ya Huduma za Habari ulipitishwa juzi na Bunge huku Waziri wa Michezo, Nape Nnauye akiwahakikishia wadau wa habari kuwa serikali itashirikiana nao katika hatua za utungwaji wa kanuni za sheria hiyo na kuwataka kuzika tofauti zao zilizojitokeza wakati wa mchakato huo.

Aidha, Serikali imefanya marekebisho 32 kwenye muswada huo ikiwamo nyongeza ya vifungu vitano vipya ambavyo viliwasilishwa na marekebisho ya kiuandishi.

Awali ulikuwa na vifungu 62 na sasa utakuwa na vifungu 67.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kupitishwa kwa sheria hiyo, Nape alisema upatikanaji wa sheria hiyo umekamilisha baada ya safari ya miaka 20.

Alisema katika mchakato huo zilionekana dalili za kuwagawa wanatasnia jambo ambalo wanapaswa kukaa na kuirudisha tasnia hiyo pamoja na kutimiza majukumu yaliyo mbele yao.

Kuhusu kanuni, alisema hatua ya utengenezaji kanuni inahitaji ushirikiano wa ili kupata kanuni zitakazofaa na kuwa na tija kwa tasnia.

Awali akijibu hoja za wabunge, Nape alisema ni lengo la sheria hiyo ni kumpunguzia Waziri mamlaka ya kutoa adhabu na kuweka maslahi bora kwa wanahabari.

Alisema muswada huo ni tofauti na Sheria ya Magazeti ya mwaka 1976 na kwamba baadhi ya wabunge walisema kila kitu kimechukuliwa kutoka sheria hiyo, jambo ambalo si kweli na kwamba yapo machache mazuri ambayo yamechukuliwa na hakuna ubaya na kwasasa sheria hiyo haimpi waziri mamlaka makubwa kama ilivyo sheria ya 1976.

Alisema serikali inataka kupunguza udhibiti wake kwa vyombo vya habari pamoja na mamlaka makubwa aliyokuwa nayo waziri kwenye Sheria ya Magazeti na ndiyo maana mamlaka hayo yamepelekwa kwenye Baraza la Habari ambako pia itaundwa kamati ya malalamiko tofauti na ilivyo sasa malalamiko yanapelekwa Idara ya Habari (Maelezo) nao wanapeleka Waziri.

“Muswada umemlinda mwanahabari kwa kumlazimisha mmiliki wa chombo cha habari kutoa mikataba ya ajira, kumkatia bima ya mazingira magumu na ya afya na kuwapo chombo cha mafunzo cha kuwaendeleza wanahabari,” alisema Nape.

Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Anastazia Wambura, alisema kwenye muswada huo vyombo vya habari pekee ndivyo vitatakiwa kukata leseni na si wanahabari.

Alisema waandishi wa habari wao watakata vitambulisho kupitia kwenye Baraza la Ithibati.

Habari Kubwa