Muuguzi asimamishwa tuhuma kumzaba makofi aliyejifungulia sakafuni

12Jan 2021
Gurian Adolf
Sumbawanga
Nipashe
Muuguzi asimamishwa tuhuma kumzaba makofi aliyejifungulia sakafuni

MUUGUZI wa zamu katika Kituo cha Afya Mazwi, mjini Sumbawanga, amesimamishwa kazi kwa tuhuma za kumpiga makofi mjamzito aliyejifungulia sakafuni akiwa katika moja ya chumba hospitalini hapo.

Taarifa zinadai mjamzito huyo (jina linahifadhiwa), alifika katika kituo hicho cha afya saa saba usiku na kupokewa na muuguzi huyo wa zamu na kupelekwa chumba maalumu kwa ajili ya kusubiri kujifungua.

Imedaiwa kuwa muda mfupi baadaye mwanamke huyo alianza kulalamika kubanwa uchungu wa kujifungua, lakini muuguzi huyo aliyetajwa kwa jina la Valentine Kinyaga, alimwambia aendelee kusubiri.

Taarifa zinadai wakati akiendelea kusubiri na uchungu ukiendelea kuongezeka, muuguzi huyo alikuwa hayupo kwenye chumba hicho, ndipo mama huyo alipoamua kutandika khanga sakafuni na kujifungua.

Taarifa zinadai kuwa baada ya kujifungua, wanawake wenzake waliokuwa katika chumba hicho wakisubiri kupelekwa kujifungua walimwita muuguzi huyo wa zamu na kukuta amejifungulia sakafuni.

Imedaiwa kuwa muuguzi huyo alianza kumpiga makofi mama huyo, huku akimfokea kwanini amejifungulia sakafuni bila kumtaarifu ili ampeleke chumba cha kujifungulia.

Baada ya kudaiwa kumpiga alianza kumsaidia kwa kumtoa mtoto na kuendelea kumpa huduma za kitabibu. Ndugu wa mjamzito huyo waliokuwa wakimsubiri ajifungue, walitoa taarifa kwa uongozi wa hospitali hiyo, na mamlaka za juu za kiutawala wa hospitali hiyo.

Mkurugenzi wa Manispaa ya Sumbwanga, Jacob Mtalitinya, alikiri kutokea kwa tukio hilo na kudai kuwa tayari wamemsimamisha kazi muguuzi huyo, ili kupisha uchunguzi wa tukio hilo.

Habari Kubwa