Muuguzi atoweka ghafla, pochi yake yakutwa chuoni

14Jun 2018
Romana Mallya
DAR ES SALAAM
Nipashe
Muuguzi atoweka ghafla, pochi yake yakutwa chuoni

MUUGUZI wa Kituo cha Afya Kerege, Bagamoyo, mkoani Pwani, Anande Mosi, ametoweka katika mazingira ya kutatanisha huku pochi yake ikikutwa imetelekezwa maeneo ya Chuo cha St. Joseph, Boko.

Ofisa Habari wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo, Veronica Luhaga, aliiambia Nipashe jana kuwa muuguzi huyo baada ya muda wa kazi, aliaga anakwenda Boko sokoni kwa ajili ya kukutana na mdogo wake.

“Aliondoka kituo cha afya saa tisa alasiri na alieleza anakwenda Boko sokoni ambako angekutana na mdogo  wake aliyekuwa anatoka nyumbani ili wanunue vitu kwa ajili ya kujiandaa kwa safari iliyopangwa kufanyika leo (jana) kwenda Tanga,” alisema.

Luhaga alisema mdogo wake alikuwa akitokea Tegeta wakati muuguzi huyo alikuwa akitokea Kerege.

Alisema mdogo wake aliwaeleza kuwa baada ya kufika sokoni eneo ambalo walikubaliana na dada yake wakutane, alikaa saa mbili bila kumwona.

“Huyu mdogo wake kazi alisema mara ya mwisho walipowasiliana na dada yake alimwambia ameshapanda gari anakwenda Boko,” alisema.

Luhaga alisema mdogo wake huyo  alipoona saa mbili zimepita na dada yake hajatokea na kwenye simu hapatikani, aliamua kuwasiliana na ndugu zake ili kuwajulisha.

Alisema baada ya juhudi kufanyika ili kujua kama wakati anatoka ofisini aliwasiliana na nani, ikabainika hakuna.

“Leo (jana) asubuhi ndiyo mlinzi wa St. Joseph akaona pochi maeneo ya chuoni na alipoipekua alikuta kitambulisho na simu ndogo lakini simu ya smartphone haipo,” alisema.

Alisema muuguzi huyo anaishi na mume wake pamoja na mdogo wake.

 

Habari Kubwa