Muuguzi kortini madai kuomba rushwa 60,000/- kusafisha kizazi

04Jun 2020
Augusta Njoji
Dodoma
Nipashe
Muuguzi kortini madai kuomba rushwa 60,000/- kusafisha kizazi

MUUGUZI wa Zahanati ya Chamwino Jijini Dodoma, Richard Zablon (32), amefikishwa mahakamani kwa tuhuma za kupokea rushwa ya Sh. 60,000 ili kutoa huduma ya kumsafisha kizazi mgonjwa.

Akizungumza jana na waandishi wa habari jijini hapa, Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa(Takukuru), Mkoa wa Dodoma, Sosthenes Kibwengo, alisema mshtakiwa huyo alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma, na kufunguliwa shauri la jinai namba 13/2020 mbele ya Hakimu Paschal Mayumba.

Alisema mshtakiwa huyo alifikishwa mahakamani hapo kwa kuomba rushwa ya Sh.100, 000 na kupokea Sh. 60,000 kinyume cha kifungu cha 15(1)(a)cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Sura ya 329 marejeo ya mwaka 2019.

“Mei 11, mwaka huu tulipokea taarifa kutoka kwa mwananchi mmoja kwamba mkewe yupo katika Zahanati ya Chamwino akihitaji huduma ya kusafishwa kizazi, lakini mshtakiwa amehitaji apatiwe fedha ndipo afanye kazi hiyo,” alisema.

Kibwengo alisema wakati mtoa taarifa bado yupo ofisini kwao, mshtakiwa huyo alimpigia simu akisisitiza apewe fedha yake kwa kuwa tayari ameshamsafisha mgonjwa.

“Lakini akaelezwa kwamba amwache mgonjwa aondoke kwani fedha zake atapelekewa, hata hivyo mshtakiwa aligoma na kuamua kuondoka na mgonjwa kwenye gari yake binafsi kwenda naye nyumbani kwa mgonjwa ili akapewe fedha,” alisema.

Alisema maofisa wa taasisi hiyo walimkamata mtuhumiwa huyo na baada ya kukamilisha uchunguzi wakamfikisha mahakamani.

Wakati huo huo, Taasisi hiyo kwa kushirikiana na Ofisi ya Mashtaka ya Mkoa wa Dodoma, inatarajiwa kumfikisha katika Mahakama ya Wilaya ya Bahi Yusufu Chuma (39), Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mpamatwa kwa tuhuma za kughushi nyaraka.

Mkuu huyo alisema mwalimu huyo anakabiliwa na makosa manne ya kugushi na kuwasilisha nyaraka zenye maelekezo ya uongo kinyume ca Sheria ya Kanuni ya Adhabu Sura ya 16 Marejeo ya mwaka 2002.

“Uchunguzi wetu umeonyesha Juni mwaka 2019 mtuhumiwa aligudhi mihtasari miwili ya vikao vya Kamati ya Shule na Mkutano wa walimu kuonyesha kwamba waliridhia kiasi cha Sh.469, 500 kitolewe kwenye akaunti ya shule na kuwasilisha kwa Mkurugenzi wa Halmashauri kuomba ridhaa yake,” alisema.

Alisisitiza kuwa fedha katika ngazi za shule hutolewa benki baada ya vikao halali kwa kuridhia ili kujua matumizi ya fedha hizo na kudhibiti ufujaji pamoja na kuboresha uwajibikaji.

Habari Kubwa