MV Mbeya kumaliza adha usafiri Nyasa

18Jun 2019
Mary Geofrey
KYELA
Nipashe
MV Mbeya kumaliza adha usafiri Nyasa

WANANCHI wa mikoa ya Ruvuma na Mbeya wanaoishi kando ya Ziwa Nyasa, wanatarajia kuanza kunufaika na usafiri wa meli ya Mv Mbeya II ambayo ujenzi wake unatarajia kukamilika Agosti, mwaka huu.

Meneja wa Bandari za Ziwa Nyasa, Abeid Gallus.

Kwa miaka miwili sasa wananchi wa maeneo hayo, hawana usafiri wa uhakika baada ya meli ya MV Songea iliyokuwa ikitoa huduma katika ziwa hilo, kusitisha safari zake tangu mwaka 2017 kutokana na kuwa na hitilafu.

Meneja wa Bandari za Ziwa Nyasa, Abeid Gallus, alisema ujenzi wa meli hiyo umefika asilimia 82.

Alisema ujenzi wa meli hiyo unagharamiwa na Mamlaka ya Bandari (TPA) kwa Sh. bilioni 9.1 na ina uwezo wa kupakia mizigo tani 200 na abiria 200 kwa wakati mmoja, hivyo kukamilika kwake itasaidia kupunguza tatizo la usafiri kwa wakazi wa mikoa hiyo.

"Kukamilika kwa ujenzi wa meli hii, kutasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza tatizo la usafiri kwa wananchi wa mikoa ya Ruvuma na Mbeya kwa sababu kwa muda mrefu walikuwa wakitumia usafiri wa boti au mashua, lakini hakuna chombo madhubuti kinachofanya kazi ziwani," alisema Gallus.

Alisema meli hiyo pia itafungua wigo wa biashara kwa nchi za Malawi na Msumbiji, hivyo kuongeza wigo na kibiashara na kuboresha uchumi wa kwa jamii zinazozungukwa na ziwa hilo.

Alisema ziwa hilo ni hatari kidogo kwa sababu lina mawimbi makubwa kwa hiyo kuwapo kwa meli hiyo kubwa kutasaidia kuimarisha usalama wa mizigo na abiria wanaokwenda sehemu mbalimbali.

Gallus alisema ujenzi wa meli hiyo ambao ulianza Julai, 2017, chini ya Kampuni ya Songoro Marine, umefikia hatua ya kufunga mitambo, kuweka vyumba, kufunga viti na umaliziaji.

Mbali na meli hiyo, alisema ziwa hilo lina meli mbili za mizigo zenye uwezo wa kubeba tani 1,000 kila moja ambazo ni MV Njombe na MV Ruvuma.

Habari Kubwa