Mvua ya upepo yaezua mapaa ya shule msingi, nyumba 33 Chalinze

20Jan 2022
Julieth Mkireri
Chalinze
Nipashe
Mvua ya upepo yaezua mapaa ya shule msingi, nyumba 33 Chalinze

MVUA iliyoambatana na upepo iliyonyesha Januari 18 imeezua mapaa ya vyumba vya madarasa mawili katika Shule ya Msingi Makombe Kata ya Lugoba Halmashauri ya Chalinze pamoja na nyumba 33.

Vyumba vya madarasa shule ya Msingi Makombe vilivyoezuliwa kwa mvua iliyoambatana na upepo.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Chalinze, Hassan Mwinyikondo akiambatana na Mkurugenzi na Kamati ya Elimu, Afya na Maji wametembelea shule hiyo na kuona athari iliyotokea.

Akiwa katika eneo hilo Mwinyikondo  amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Ramadhani Posi kuhakikisha Mhandisi anafika mapema kufanya tathmini ili wanafunzi waendelee kutumia vyumba hivyo.

Mkurugenzi Posi amesema  kupitia mapato ya ndani wamekuwa wakitenga fedha kwa ajili ya sekta ya elimu hivyo kufuatia maafa hayo wataalamu watafika kufanya tathmini  na ukarabati utafanyika mapema.

Kuhusu nyumba zilizoezuliwa amesema watajadiliana na Baraza la Madiwani kuona ni mahitaji gani wanaweza kusaidia.

Afisa Elmu Msingi Miriam Kihiyo amesema kwasasa wanafunzi wa shule ya makombe wanasoma kwa awamu katika kipindi hiki ambacho wanasubiri vyumba hivyo kukarabatiwa.

Diwani wa Lugoba Rehema Mwene amesema wananchi ambao nyumba zao zimeezuliwa wamehifadhiwa kwa majirani.

Habari Kubwa