Mvua ya upepo yaua, yakosesha watu makazi

07Dec 2021
Neema Hussein
Katavi
Nipashe
Mvua ya upepo yaua, yakosesha watu makazi

MTOTO mmoja mwenye umri wa mwaka mmoja na nusu amefariki dunia na mwingine kujeruhiwa baada ya kuangukiwa na ukuta wa nyumba kutokana na mvua kubwa iliyoambatana na upepo.

Tukio hilo lilitokea Desemba 4, katika Kijiji cha Muungano na Kashelami Halmashauri ya Nsimbo, mkoani Katavi.

Akizungumza na Nipashe Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Katavi, Ali Hamad alisema, kaya zaidi ya 40 zimekosa makazi na makanisa mawili kuezuliwa.

Hamad alisema mpaka sasa kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa inakusudia kufika katika eneo la tukio na kuangalia jinsi ya kuwasaidia waathirika wa tukio hilo ambao wamehifadhiwa kwa ndugu, jamaa na marafiki.

Hata hivyo, Hamad alisema nyumba hizo hazikuwa na miundombinu imara ya kuhimili mvua na upepo na kutoa wito kwa wananchi kujitahidi kujenga nyumba imara ili kuepukana na matatizo kama hayo.

Kwa upande wake Annastazia John, shuhuda wa tukio hilo alisema ilikuwa muda wa saa 12 jioni, mama wa mtoto huyo alipomaliza kumwogesha na kumweka ndani ya nyumba yao baada ya mvua kuanza alitoka nje kufunga mlango wa chumba kingine na aliporudi ndani alikuta mtoto tayari kaangukiwa na ukuta huo.

Annastazia alisema baada ya mama mtu kuomba msaada kwa majirani walimtoa mtoto huyo na kumpeleka hospitali hadi umauti ulipomkuta.

Habari Kubwa