Mvua yaharibu nyumba 260 Njombe, Morogoro

22Jan 2022
Na Waandishi Wetu
Njombe
Nipashe
Mvua yaharibu nyumba 260 Njombe, Morogoro

MVUA kubwa iliyoambatana na upepo imesababisha maafa katika vijiji viwili kwenye mikoa ya Njombe na Morogoro kwa kuezua takriban nyumba 260 na kujeruhi watu wawili.

Katika kijiji cha Banawanu mkoani Njombe, nyumba 27 zimeezuliwa na watu wawili kujeruhiwa huku mkoani Morogoro, nyumba 230 zimeezuliwa katika kijiji cha Kisegese, Halmashauri ya Mlimba.

Akizungumza katika Kamati ya Tathimini ya Maafa ya Halmashauri ya Wilaya ya Wanging’ombe, Mwenyekiti wa Kijiji cha Banawanu, Watson Mwenda, alisema tukio hilo lilitokea juzi majira ya saa 10:00 jioni. Mwenda aliwataja majeruhi kuwa ni Amos Kuyava (45) na Faraja Site (2).

Alisema mvua hizo pia zimeleta maafa katika Kitongoji cha Talibato na kwamba katika vitongoji vingine baadhi ya nyumba zimedondoka.

"Kijiji chetu kina vitongoji vitano lakini kilichoathirika sana ni Kitongoji cha Talibato nyumba 21, Mji Mwema nyumba tatu, Banawanu Kati kumeezuliwa nyumba mbili, Nyaubaga nyumba moja kwa hiyo kwa jumla nyumba zote zilizoezuliwa ni 27,"alisema Mwenda.

"Mvua hizo zimeleta athari pia kwa kujeruhi watu wawili mmoja ni mtu mzima ambaye ameumia na mwingine ni mtoto ambaye amepelekwa Hospitali ya Ikelu lakini anaendelea na matibabu. Hakuna aliyefariki dunia ila watu nyumba zao nyingi zimeezuliwa mapaa na zingine zimebomoka kabisa,” aliongeza.

Wakizungumza na Nipashe, baadhi ya waathirika wa tukio hilo akiwamo Beatrice Mtivike, waliiomba serikali kuwasaidia chakula na sehemu ya kulala.

"Mimi sina pa kulala nalala jikoni ambako hakuna mlango, nilikua nimeweka mahindi yangu lakini yote yamekwenda na maji pamoja na nguo kwa kweli naiomba serikali itusaidie ione namna ya kutusaidia kwa sababu hili janga limetukuta katika kipindi kigumu,” alisema Mtivike.

Hata hivyo, alimshukuru Mungu kwa kunusurika katika tukio hilo kwa sababu wakati linatokea alikuwa shambani.

Mwathirika mwingine, Abel Kidegelime, alisema kuezuliwa kwa nyumba yake kumemwathiri kutokana na kupoteza chakula na baadhi ya vifaa kuharibika.

Geofrey Benela alisema tukio hilo limewakuta kipindi ambacho ni cha maandalizi ya kuwapeleka watoto shuleni.

"Janga hili limetukuta kipindi ambacho tunatakiwa kuwapeleka watoto shule, limetudhoofisha sana kimaisha, upepo ulikua mkali ndiyo maana imeleta madhara makubwa,” alisema Benela.

Ofisa Mazingira wa Wilaya ya Wanging'ombe, Frank Ngogo, alitoa pole kwa kaya zilizokutwa na maafa hayo na kuwataka kuwa watulivu katika kipindi hiki.

MAAFA MLIMBA

MVUA iliyoambatana na upepo mkali imeezua nyumba zaidi ya 230 katika kijiji cha Kisegese, Halmashauri ya Mlimba, Kilombero mkoani Morogoro na kuwaacha baadhi ya wakazi bila mahali pa kuishi.

Baadhi ya waathirika, wakiwamo Zainab Mpendi na Victor Komba, walikiri kuwa hali zao ni mbaya kutokana na maafa hayo, ambayo yamewafanya baadhi ya wananchi kulala nje na wengine kuhifadhiwa na majirani.

Walisema upepo mkali uliibuka wakati mawingu yalipokuwa yakijipanga kunyesha mvua na kusababisha baadhi ya nyumba kuezuliwa mapaa.

“Hali ilikuwa mbaya. Nilikuwa natokea shambani kwangu manyunyu ya mvua yakiendelea kunisindikiza. Nilipokaribia kijijini, ghafla ulianza upepo mkali ambao ulisababisha tawi la mti karibu yangu kukatika. Nilipofika nyumbani nikakutana na majanga mengine ya nyumba kuezuliwa paa," alisema Mpendi.

Mbunge wa Mlimba, Godwin Kunambi, jana alifika kijijini hapo na kushuhudia mazingira ya nyumba zilizoezuliwa na kuwasaidia wananchi waliokuwa katika hali mbaya zaidi Sh. milioni mbili na kuahidi kujenga nyumba ya  moja ya wananchi ambaye ni mgonjwa.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Kisegese, Manfred Meyambe, alisema hatua walizozichukua baada ya athari hizo ni pamoja na kuhakikisha wanahifadhi wanakijiji waliokuwa na hali mbaya ya kimakazi na kuandaa maeneo ya wazi kwa ajili ya hifadhi.

“Tumefuatilia zaidi ya nyumba 230 zilizopata athari za upepo na tunashukuru kupata msaada kutoka serikalini na kwa mbunge wetu Godwin Kunambi. Mpaka sasa hakuna jambo lililokwama japo bado wananchi wanahitaji msaada zaidi wa kibinadamu," alisema.

Imeandikwa na Na Elizabeth John, NJOMBE na Iddah Mushi, MLIMBA.

Habari Kubwa