Mwakilishi ajiengua mbio za urais Zanzibar

30Jun 2020
Na Mwandishi Wetu
Zanzibar
Nipashe
Mwakilishi ajiengua mbio za urais Zanzibar

MWAKILISHI wa Jimbo la Mtoni Ibrahim Makungu ambaye ni miongoni mwa wanachama 32 wa CCM waliochukua fomu ya kugombea urais wa Zanzibar amejitoa katika kinyang’anyiro hicho.

Akizungumza na waandishi wa habari Ofisi Kuu ya CCM Kisiwandui, alisema ameamua kufanya hivyo kutokana na baadhi ya wagombea waliojitokeza kuwa na uwezo mkubwa na sifa kuliko yeye.

Alisema pia sababu nyingine ya kujiengua katika kinyang’anyiro hicho ni wananchi wa Jimbo la Mtoni bado wanamuhitaji katika masuala mbalimbali ya kimaendeleo.

Alieleza kuwa uamuzi wake huo utakirahisishia chama kufanya kazi zake katika kuwajadili wagombea hao katika vikao vyake mbalimbali.

“Kwa sasa nitaendelea kushiriki kugombea nafasi ya uwakilishi katika jimbo langu kwani bado wananchi wananihitaji, na nimeshajipanga vizuri kuhakikisha nawawekea mazingira mazuri wanafunzi hasa wa usafiri,” alisema.

Ibrahim alieleza kuwa hajashawishiwa na mtu yeyote kujitoa katika kinyang’anyiro hicho bali ni uamuzi wake katika kupunguza muda katika kujadili wagombea katika vikao vinavyotarajiwa kufanyika hivi karibuni.

Alisema atahakikisha anashirikiana na mgombea urais atakayeteuliwa na chama katika kukipatia ushindi chama hicho katika uchaguzi mkuu.

Katika hatua nyingine idadi ya wagombea waliorejesha fomu imefikia 24 ambapo jana wagombea watano walirejesha akiwamo Jecha Salum Jecha, Perera Ame Silima, Bakar Rashid Bakar, Hasna Attai Masoud na Mussa Aboud Jumbe.

Akizungumza baada ya kurejesha fomu hiyo Hasna Attai Masoud alisema anasubiri maamuzi ya chama na kuwataka wanawake kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali za uongozi badala ya kusubiri nafasi za kuteuliwa.

Wagombea 32 waliochukua fomu ni Mbwana Bakari, Balozi Ali Karume, Mbwana Mwinyi Yahya, Omar Shehe, Muhammed Jafar, Muhammed Hija, Meja Jenerali Issa Suleiman Nassor, Shamsi Vuai Nahodha na Dk. Hussein Mwinyi.

Wengine ni Profesa Makame Mbarawa, Mwatum Mussa Sultan, Haji Rashid Pandu na Dk. Abdul-halim Mohammed Ali, Jecha Salim Jecha na Dk. Khalid Salum Muhamed.

Wengine ni Rashid Ali Juma, Khamis Mussa, Mmanga Mjengo Mjawiri, Hamad Yussuf Masauni, Muhammed Aboud, Bakari Rahid, Ibrahim Makungu, Ayoub Muhammed Mahmoud, Hashim Salum Hashim na Hasna Ataai Maoud.

Wamo pia Fatma Kombo Masoud, Pereira Ame Silima, Iddi Hamad Iddi, Shaame Ame Silima, Mussa Aboud Jumbe, Mgeni Hassan Juma na Maudline Castico.

Habari Kubwa