Mwakyembe agundua mawakili makanjanja

24Nov 2016
Chauya Adamu
Dar es Salaam
Nipashe
Mwakyembe agundua mawakili makanjanja

WAZIRI wa Katiba na Sheria, Dk. Harrison Mwakyembe, amesema serikali imebaini kuwapo kwa wasaidizi wa masuala ya kisheria 80,000 ambao hawana ujuzi, akiwaita ni "makanjanja".

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Dk. Mwakyembe alisema ni vyema watu hao wakaenda kusoma kabla serikali haijawafikia.

Waziri huyo alisema imefikia mahali wananchi wanashindwa kuwaamini watoaji wa misaada ya kisheria na hivyo kuwataka wananchi kutambua wale waliosajiliwa na serikali.

Aidha, katika kuhakikisha serikali inafanya vyema kwenye masuala ya kisheria, Dk. Mwakyembe amewataka wanasheria wenye elimu ya ngazi za cheti katika mahakama za mwanzo kuachia nafasi hizo na kwamba mpango wa serikali ni kuwa na wanasheria wa ngazi za Stashahada (Diploma) na kuendelea.

Alisema kama wanasheria hao wanataka kuendelea na kazi hiyo, wanatakiwa kwenda kuongeza kiwango cha elimu waliyonayo ili kuboresha utoaji wa huduma za kisheria kwa wananchi.

“Katika mahakama zetu za mwanzo tutawaondoa wanasheria wote wenye vyeti na kwamba ili kuboresha utoaji wa huduma za kisheria, tunahitaji wanasheria wenye elimu ya diploma (stashahada) na kuendelea,” alisema Dk. Mwakyembe.

Aidha, kiongozi huyo wa serikali alisema kutokana na wananchi wengi kukosa misaada ya kisheria, serikali inatarajia kuwa na sheria ya usaidizi wa kisheria kwa wananchi wa hali ya chini na kuwatambua rasmi wasaidizi wa kisheria watakaotoa huduma hiyo kupitia sheria hiyo.

Alisema hadi sasa, jumla ya wasaidizi wa sheria 5,000 wamesambazwa nchi nzima katika kila wilaya na kwamba hao ndiyo wanaotambuliwa na serikali.

Alisema wasaidizi hao wanaotambuliwa na serikali walipata mafunzo ya wiki tatu, hivyo wana ujuzi wa masuala ya kisheria tofauti na wengine aliowaita makanjanja.

Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi wa Sheria wa wizara hiyo, Felista Joseph, alisema Muswada wa Sheria ya Msaada wa Sheria ulisomwa kwa mara ya kwanza bungeni Novemba 10 mwaka huu.

UKO MIKONONI
Alisema unalenga kutoa huduma za kisheria kwa wananchi wa hali ya chini na kwamba utapelekwa kwa wananchi na wadau wengine wa mambo ya sheria ili watoe maoni yao kuona ni namna gani unaweza kuwa msaada kwa wale watakaokosa misaada ya kisheria.

“Muswada huu umepitia ngazi zote za uamuzi ndani ya serikali na sasa uko mikononi mwa mamlaka ya Bunge na lengo la muswada huu ni kuwasaidia wananchi wa hali ya chini wasioweza kumudu gharama za mawakili.

Tutatoa fursa kwa wananchi na wadau wa masuala ya kisheria waujadili kabla ya kurudi bungeni kwa mara ya pili ili tuone ni kwa namna gani unaweza kuwasadia wananchi," alisema.

Aliongeza kuwa muswada huo ni matokeo ya mjadala uliofanyika ndani ya miaka mitatu ili kujua namna ya kumfikia mwananchi asiyetambua jinsi ya kupata haki zake katika jamii na kwamba serikali itaandaa majarida maalumu ya kutoa elimu ya kisheria kwa wananchi kujua haki zao.

Alisema wananchi wengi wanashindwa kujua haki zao za msingi kutokana na sheria zote kuandikwa kwa lugha ya Kiingereza na kukosa ufafanuzi ambapo serikali kupitia muswada huo itahakikisha sheria zinakuwa kwa lugha za Kiswahili na Kiingereza.

Alisema serikali inaendelea na juhudi kuhakikisha upatikanaji wa haki za raia wake ikiwa ni pamoja na watu maskini na makundi maalumu ya watu wasio na uwezo wa kugharamikia mawakili na kwamba kila mtu apate haki yake bila vikwazo.

Habari Kubwa