Mwakyembe akerwa uharibifu maeneo muhimu ya kihistoria

15Mar 2019
Na Mwandishi Wetu
Tabora
Nipashe
Mwakyembe akerwa uharibifu maeneo muhimu ya kihistoria

SERIKALI imekemea tabia ya kuharibu maeneo ya kihistoria yakiwamo majengo ya kale kwa madai potofu kuwa wakoloni walificha madini ndani yake.

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe, picha mtandao

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe, alisema hayo jana wakati wa ziara yake katika Manispaa ya Tabora kutembelea maeneo ya urithi wa ukombozi wa bara la Afrika.

Alisema vitendo vya aina hiyo vinasababisha serikali kutumia gharama kubwa pindi inapotaka kukarabati na kurudisha historia ya maeneo hayo.

“Hakuna ambaye ni mjinga aweke ndani ya nyumba dhahabu halafu asiifuate. Hata wangekuwa wameweka mali ndani ya majengo yao wangekuja na njia nyingine ya kutaka kuendeleza maeneo hayo kwa kuweka miradi ya kuchimba visima ili wachukue madini kama yangekuwapo” alisema.

Dk. Mwakyembe alisema maeneo hayo ni muhimu sana katika historia ya Tanzania na pia katika ukuzaji wa utalii kwa ajili ya kulipatia taifa fedha za kigeni.

Aliongeza kuwa maeneo hayo ni muhimu katika kutoa elimu kwa vijana wa kitaifa kufahamu historia ya nchi yao kwa ajili ya kuwa wazalendo wazuri wa Tanzania.

Mwakyembe alisema wizara yake inaendelea na utaratibu wa kuyaorodhesha maeneo yote ya kihistoria kwa ajili ya kuyahifadhi na kuyakarabati kwa ajili faida ya kizazi cha sasa na kijacho.

Aidha, alisema serikali iko mbioni kupeleka bungeni muswada wa sheria ambayo utafanya maeneo ya kihistoria yasiguswe na kuzuia uharibifu.

Alisema baada ya muswada huo kupitishwa na hatimaye kuwa sheria utasaidia kulinda utajiri wa urithi wa kihistoria ulipo hapa nchini usiweze kuharibiwa na kupotea.

Katika hatua nyingine, Dk. Mwakyembe alisema serikali itahakikisha inarudisha nchini Fuvu la Kichwa cha Mama Shujaa Mpiga Ukoloni wa Kijerumani kutoka Singida, Bibi Liti.

Alisema Shujaa huyo alipambana na Wajerumani kwa kutumia nyuki hadi aliposalitiwa na wenzake na hatimaye Wajerumani wakakata kichwa chake na kuondoka nacho.

Dk, Mwakyembe alisema lazima fuvu la kichwa lirudishwe nchini na kuhifadhiwa katika jumba maalumu kwa ajili ya historia ya Tanzania
 

Habari Kubwa