Mwalimu kizimbani tuhuma kupokea rushwa 600,000/-

20Jul 2021
Renatha Msungu
Dar es Salaam
Nipashe
Mwalimu kizimbani tuhuma kupokea rushwa 600,000/-

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoani Dodoma, imemfikisha mahakamani Kaimu Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mafurungu wilayani Chamwino, Malisero Saveli (29), kwa tuhuma za kuomba rushwa ya Sh. 600,000 ili asimchukulie hatua mwanafunzi mtoro.

Saveli ambaye ni Kaimu Mtendaji wa Kijiji cha Ilangali wilayani humo, alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma kwa madai ya kutomchukulia hatua mwanafunzi wa darasa la nne.

Kwa mujibu wa taarifa ya Mkuu wa Taasisi hiyo Mkoa wa Dodoma, Sosthenes Kibwengo, mtuhumiwa huyo aliomba rushwa ya Sh.600,000 na kupokea Sh. 400,000 kutoka kwa mtoa taarifa ili asimchukulie hatua mwanafunzi huyo kwa kitendo cha utoro wa mtoto.

Kibwengo alisema kitendo cha mwalimu kudiriki kuomba na kupokea rushwa ni kwenda kinyume cha taaluma yake kwa kukwamisha elimu badala ya kuchochea elimu.

Alisema mtuhumiwa huyo amefunguliwa mashtaka mawili ya kushawishi na kupokea rushwa kinyume cha Kifungu cha 15 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Sura ya 329 Marejeo ya 2019.

Mkuu huyo alisema elimu ni ufunguo wa maisha na serikali kila kukicha inasisitiza kuwekeza zaidi katika elimu ikiwamo kuimarisha mazingira ya utoaji elimu.