Mwalimu mbaroni tuhuma kubaka mwanafunzi wake

26Mar 2020
Gurian Adolf
Nkasi
Nipashe
Mwalimu mbaroni tuhuma kubaka mwanafunzi wake

MWALIMU wa Shule ya Sekondari Milundikwa, Kata ya Nkandasi wilayani Nkasi mkoani Rukwa, anashikiliwa na polisi mkoani humo kwa tuhuma za kumbaka mwanafunzi wa kidato cha pili (17) katika shule hiyo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, Justine Masejo, alidai jana kuwa tukio hilo lilitokea Machi 15 mwaka huu majira ya usiku, mwalimu huyo (37), akidaiwa kumbaka mwanafunzi wake katika nyumba ya kupanga ambayo mwanafunzi huyo alikuwa anaishi.

Ofisa Mtendaji wa Kijiji iliko shule hiyo, Benazir Kalamba, alidai ofisi yake ilipata taarifa kuwa mwanafunzi huyo amebakwa na mwalimu wake usiku majira ya saa sita, na baada ya kuzipata, naye akatoa taarifa kwa Ofisa Elimu wa Wilaya ya Nkasi ili hatua za kisheria zichukuliwe.

Alidai Ofisa Elimu alitoa taarifa kwa Jeshi la Polisi ndipo mwalimu huyo akakamatwa na mpaka sasa anashikiliwa na jeshi hilo wakati upelelezi ukiendelea.

Makamu Mkuu wa Shule hiyo, Charles Mwamengo, alisema tukio hilo limejitokeza ikiwa ni siku chache baada ya uongozi wa shule hiyo kuketi kikao na walimu na kuwaonya kuhusu tabia ya kujihusisha kimapenzi na wanafunzi.

Alisema kwa muda mrefu kumekuwa na taarifa kuwa baadhi ya walimu wa shule hiyo wamekuwa na tabia ya kujihusisha na mapenzi na wanafunzi wao.

Habari Kubwa