Mwalimu mmoja afundisha shule nzima wanafunzi 366

02Jul 2019
Na Mwandishi Wetu
KAHAMA
Nipashe
Mwalimu mmoja afundisha shule nzima wanafunzi 366

MWALIMU wa Shule ya Msingi Mikwa Kata ya Mapamba Halmashauri ya Ushetu mkoani Shinyanga, Elias Zabron, ameiomba serikali kuongeza walimu hasa wa masomo ya sayansi katika shule hiyo yenye zaidi ya wanafunzi 366 na mwalimu mmoja.

Shule hiyo ilianzishwa na wazazi baada ya wanafunzi waliokuwa wakisoma katika Shule ya Msingi Mapamba kuwa mbali kwa zaidi ya kilometa 15, huku baadhi walilazimika kwenda kusoma katika shule za msingi zilizopo Halmashauri ya Uyuwi mkoani Tabora.

Zabroni aliyabainisha hayo alipotembelewa na maofisa kutoka mpango wa kuinua ubora wa elimu Tanzania (EQUIP) kukagua ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa na ofisi moja ya walimu vilivyokuwa vikijengwa kwa fedha kutoka katika mfuko huo.

Alisema shule hiyo ina zaidi ya wanafunzi 366, madarasa matatu na ofisi moja ya walimu huku ikiwa na wanafunzi kuanzia darasa la awali mpaka la tatu na kudai kuwa amekuwa akiwafundisha kwa awamu, hivyo kusababisha wengi wao kutojua kusoma na kuandika.

Aidha, Zabron, alisema akifundisha siku moja siku inayofuata anajikita katika kusahihisha madaftari ambayo huchukua siku tatu hadi kumaliza, na siku zote hizo wanafunzi wanakosa masomo na kuendelea kucheza nje hadi mwisho wa vipindi.

“Shule hii ina zaidi ya wanafunzi 366 kuanzia darasa la awali hadi darasa la tatu na nimekuwa nikifundisha mwenyewe, na wakati mwingine nawapatia vitabu wanafunzi wa darasa la tatu wenye uelewa na kwenda kufundisha darasa la kwanza na awali,” alisema Zabron.

Aliongeza: “Kulikuwa na mwalimu mmoja wa kujitolea na alikuwa analipwa shilingi 500 na kila mzazi mwenye mtoto, lakini ameshindwa kuendelea kufundisha kutokana na kutolipwa kwa zaidi ya miezi mitatu, na ninapoumwa hata ikichukua miezi miwili wanafunzi wanakosa masomo.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Ushetu, Michael Matomora, alikiri shule hiyo kuwa na mwalimu mmoja ambae anafundisha kuanzia darasa la awali hadi la tatu, na kuongeza kuwa mwezi huu ataongeza walimu wengine watatu ili kwenda kusaidia ufundishaji.

Aidha, alisema shule hiyo ni moja kati ya shule shikizi zilizosajili na kuwa shule za msingi kamili baada ya EQUIP kujenga vyumba viwili vya madarasa na ofisi moja ya walimu katika Shule ya Msingi Mikwa, Kawekamwe na Mliza.