Mwalimu mmoja afundisha wanafunzi 242

17Feb 2020
Jaliwason Jasson
Manyara
Nipashe
Mwalimu mmoja afundisha wanafunzi 242

SHULE Shikizi ya Maweni, Halmashauri ya Babati mkoani Manyara, yenye wanafunzi 242 na madarasa manne ina mwalimu mmoja pekee.

waziri wa elimu, prof. joyce ndalichako, picha mtandao

Mwalimu wa Mkuu wa shule hiyo, Jacob Mwenda, alitoa taarifa hiyo wakati akizungumza na Kamati ya Siasa ya Wilaya ya Babati na wananchi.

Mwalimu Mwenda alisema shule hiyo ina madarasa ya awali hadi darasa la tatu huku masomo yote akifundisha peke yake.

Alisema darasa moja anaweza kufundisha masomo mawili ili kila mwanafunzi aweze kuambulia kitu.

"Naiomba serikali inisaidie kuongeza walimu angalau tuwe wanne ili tuweze kufundisha wanafunzi hawa," alisema Mwalimu Mwenda.

Mmoja wa wananchi akizungumza na Nipashe kuhusu uhaba wa walimu kwenye shule hiyo, Rukia Kemo, alisema kwa hali hiyo uwezekano wa watoto kufanya vizuri ni mgumu.

Aliiomba serikali kuongeza walimu kwenye shule hiyo kwa kuwa wanahitaji watoto wao wafanye vizuri kwenye masomo na kufaulu.

Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Filbert Mpwepwe, akizungumza na wananchi hao aliwataka viongozi wa Kijiji cha Endadosh na Kata ya Qash kuongeza jitihada ili shule hiyo ikamilike haraka.

Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Babati, Nicodemus Tarimo, alisema wananchi wa kijiji hicho hawajitumi licha ya halmashauri kuwachangia Sh. milioni tano.

Tarimo alisema ili shule iweze kupata usajili ni lazima iwe imekamilisha ujenzi wa miundombinu kwa asilimia 75.

Alimtaka diwani wa kata hiyo kuwachukulia hatua wenyeviti wa vitongoji wanaokula fedha ya michango ya wananchi badala ya kulalamika.

Diwani wa Kata ya Qash, John Kanda, alidai kinachokwamisha ujenzi wa shule hiyo ni fedha kutafunwa.

Habari Kubwa