Mwalimu mstaafu auawa,atupwa kando barabarani

23Jan 2022
Gideon Mwakanosya
Songea
Nipashe Jumapili
Mwalimu mstaafu auawa,atupwa kando barabarani

​​​​​​​MWALIMU mstaafu Kassim Shiraz (67), amekutwa akiwa ameuwawa na watu wasiojulikana na mwili wake kutupwa pembezoni mwa barabara ya Songea- Mbinga.

Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma, Pilli Mande.

Kutokana na mauaji hayo, Jeshi la Polisi mkoani Ruvuma linamsaka mtu mmoja aliyetajwa kwa jina la Kamongo, fundi seremala, mkazi wa  mtaa wa Namanditi katika Manispaa ya Songea.

Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma, Pilli Mande,  alisema tukio hilo lilitokea jana majira ya saa 12:00 asubuhi katika  mtaa wa Namanditi kwenye  stendi ya mabasi iliyoko kata ya Ruhuwiko.

Kamanda Mande alisema siku hiyo ya tukio kwenye kituo cha mabasi cha Namanditi,  Shiraz ambaye alistaafu kazi mwaka 2018, alikutwa akiwa ameuawa pembezoni mwa barabara akiwa amechomwa na kitu chenye ncha kali maeneo ya mgongoni.

Alisema chanzo cha mauwaji ni wivu wa mapenzi kwa madai kwamba Mwalimu Shiraz tangu mwaka 2017 alikuwa na uhusiano na mwanamke mmoja (jina linahifadhiwa) ambaye fundi seremala huyo alianza kumfuatilia na kumtaka uhusiano wa kimapenzi lakini akamkataa kwa madai kuwa ana mpenzi wake ambaye ni Shiraz.

Kamanda Mande alisema fundi Kamongo alimtishia kwa maneno mwalimu huyo mstaafu kuwa atamuuwa jambo ambalo lilimlazimu kutoa taarifa ya kutishiwa kwa maneno katika kituo kidogo cha polisi cha Madizini kata ya Lizaboni.

Alisema mazingira yanaonyesha kuwa mwanamke huyo hivi karibuni alianza kuwa na uhusiano wa kimapenzi na fundi Kamongo na kwamba juzi  usiku, majira kati ya saa 3:00 na saa 4:00  usiku, walikuwa kwenye baa moja wote watatu wakipata vinywaji na  Mwalimu Shiraz alitoka na huyo mwanamke huku fundi akiondoka peke yake.

Kamanda alisema pamoja na watu hao kuondoka kwa njia tofauti, siku ya pili Shiraz alikutwa akiwa ameuawa na kutupwa kando ya barabara na mwili wake ukiwa umechomwa na kitu chenye ncha kali.

AHOJIWA TUHUMA MAUAJI

Katika hatua nyingine, Polisi mkoani Ruvuma wanamshikilia mwendesha pikipiki (jina linahifadhiwa) kwa mahojiano kutokana na mauaji ya kikatili  ya Gema Haule (23), mkazi wa mtaa wa Kimoro Makambi, Manispaa ya Songea, aliyekuwa mhudumu wa nyumba ya kulala wageni ya Peace Lodge iliyoko Matarawe.

Kamanda Mande alisema jana kuwa kufuatia tukio lililotokea juzi la mauwaji ya kikatili tayari polisi ilishaanza kufanya jitihada za kuhakikisha kuwa mtuhumiwa wa mauwaji hayo anakamatwa.

Alisema upelelezi wa awali wa polisi umebaini kuwa mtuhumiwa huyo baada ya kumuuwa kikatili Gema kwa kumkaba shingo kisha kumfunga shingoni na kamba za viatu na hivyo kumsababishia kifo, alichukuwa ufunguo wa chumba ambako alifanyia kitendo hicho cha kinyama na kukifunga.

Kamanda Mande alisema upelelezi umebaini kuwa baada ya kuua, mtuhumiwa alichukua nguo, simu zilizokuwa zimechukuliwa na mhudumu baada kushindwa kulipa deni la pango la Sh. 50 kisha alichukuwa kitabu cha wageni na kuchana ukurasa ambao una taarifa zake likiwamo jina kamili la mtuhumiwa.

Alisema mtuhumiwa huyo aliondoka eneo la tukio kwa usafiri wa bodaboda akiwa na ufunguo wa chumba namba 4 ambacho alikuwa amemfungia mhudumu wa nyumba hiyo na kutokomea hadi eneo la kituo cha daladala cha Majengo wakati simu moja aliiacha kwa mmiliki wa gesti hiyo.

Mande alisema mtuhumiwa huyo akiwa eneo la Majengo, alimwomba mwendesha bodaboda amsaidie kurudisha ufunguo wa chumba ambao alidai kuwa aliondoka nao kwa kutokujua na mwendesha bodaboda alikubali na kuuchukua ufunguo na kwenda nao hadi kwenye nyumba hiyo ambako alipofika, alikuta umati mkubwa wa watu wakiwamo askari polisi waliokuwa wamefika baada ya kusikia tukio hilo.

Alisema dereva huyo alikabidhi ufunguo akidai kuwa amekabidhiwa na mteja wake aliyedai kuwa amesahau kuurudisha kisha polisi walimkamata kwa lengo la kusaidia upelelezi.

Kamanda alisema baada ya mahojiano, polisi wamejiridhisha na kumwachia kwa kuwa  alikuwa hafahamu chochote kuhusiana na tukio hilo licha ya kuwa alimbeba mteja wake ambaye aliomba ampeleke majengo na baadaye kuomba amsaidie kurudisha ufunguo jambo ambalo limeonyesha kuwa hakukuwa na sababu ya kuendelea kumshikilia.

Januari 18, mwaka huu, majira ya saa 10:00 katika maeneo ya nyumba ya kulala wageni ya Peace Lodge, Gema Haule (23) ambaye alikuwa mhudumu wa gesti hiyo, alikutwa ameuwawa kikatili kwa kukabwa shingoni na kamba za viatu na mpangaji wake alikuwa anadaiwa Sh. 50,000 za pango la siku tano.

Habari Kubwa