Mwambe aanika   ‘mchawi’ biashara

19Dec 2020
Paul Mabeja
DODOMA
Nipashe
Mwambe aanika   ‘mchawi’ biashara

WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Geoffrey Mwambe, amesema kuwa moja ya vikwanzo vinavyosababisha Watanzania kushindwa kupiga hatua kwenye biashara ni ukosefu wa elimu ya ujasiriamali.

WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Geoffrey Mwambe.

Mwambe aliyasema hayo jana jijini hapa alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari baada ya kufungua mkutano wa wadau kuhusu rasimu ya Sera ya Maendeleo ya Viwanda Vidogo na Biashara Ndogo.

Alisema pamoja na matatizo ya ukosefu wa masoko ya bidhaa mbalimbali na mitaji, elimu bado ni kikwazo kikukwa kwa Watanzania katika kuanzisha biashara zao.

“Watanzania bado hii elimu ya ujasilimali ni suala geni kidogo kwetu, leo hii Mtanzania anakwenda chuo cha biashara kusoma ili aje kuwa msimamizi wa biashara ya mtu na si kubuni yake, ”alieleza Mwambe.

Kutokana na hali hiyo, alivitaka vyuo vya elimu ya biashara nchini pamoja na taasisi mbalimbali kuweka utaratibu wa kutoa mafunzo ya ngazi mbalimbali ili kuwajengea uwezo watu kwenda kuanzisha biashara zao.

“Leo hii unakuta Chuo cha Elimu ya Biasahra (CBE) kinafundisha mtu kwenda kuwa msimamizi wa biashara ya kampuni fulani lakini yeye mwenyewe si mfanyabiashara. Inabidi tubadilike. Hivi karibuni nilikutana na Mo Dewji akanambia anasoma shahada ya uzamili ya biashara Dubai. Hata sisi wajasiriamali wadogo lazima tusome ili kuwa wafanyabiashara na si wasimamizi,” alisisitiza.

Kuhusu rasimu hiyo ya sera ya maendeleo ya viwanda vidogo na biashara ndogo, aliwata wajumbe wa mkutano huo kufanya maboresho ili ipatikane sera itakayosaidia sekta hiyo.

“Lazima mtoke na maboresho ya sera ambayo itakwenda kutambua viwanda vidogo pamoja na biashara ndogo kwani ndizo ambazo zimewatoa watu wengi mtu kama Bakharesa alianza na kutembeza mikate lakini hivi sasa ni tajiri mkubwa” alisema.

Pia alisema serikali imekuja na rasimu ya sera hiyo kutokana na iliyokuwapo awali kuwa ya muda mrefu na haikidhi mahitaji ya sasa.

Alisema sera ya ujasiriamali ni ya mwaka 2003 ni siku nyingi sana inatakiwa kufanyiwa marekebisho ili kwenda kisasa.

“Lakini changamoto nyingine katika sera ile ya awali ni ilijengwa katika malengo ya sekta moja tu ya viwanda ndiyo maana akawa zaidi chini ya SIDO, lakini hivi sasa biashara ndogo zipo katika sekta zingine pia kama vile hoteli,” alisema.

Mwambe alisema sera hiyo mpya itakuwa na uwezo wa kuwawezesha wajasiriamali wadogo kukua kutoka ngazi ya chini na kuwa wafanyabiasahra wakubwa hali itakayosaidia kuongeza walipa kodi na taifa kupata mapato.

Habari Kubwa