Mwanafunzi abakwa, auawa na hatimaye akitobolewa macho

02Dec 2021
Hamisi Nasiri
Masasi
Nipashe
Mwanafunzi abakwa, auawa na hatimaye akitobolewa macho

MWANAFUNZI wa darasa la sita katika Shule ya Msingi Maendeleo Wilaya ya Masasi mkoani Mtwara, Zinati Alifa (13), amebakwa, kuuawa kisha maiti yake kutupwa kwenye mapango ya miamba ya Mto Kabomola.

Aidha, mwili wa mwanafunzi huyo ambaye ni mkazi wa mtaa wa Mchema Kata ya Mkomaindo, ulikutwa umetobolewa macho na kitu chenye ncha kali.
 
Akizungumza na gazeti hili, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mchema, Shaibu Chande, alisema mwili huo uliokotwa juzi ukiwa umefichwa kwenye miamba hiyo.
 
Alisema kabla ya kufikwa na umauti, mwanafunzi huyo Septemba 26, mwaka huu majira ya saa 11:30 jioni aliwaaga wazazi wake kuwa anakwenda kuokota korosho na maembe kwenye mashamba yaliyopo eneo la Mchemba kilomita chache kutoka kwao.
 
“Mwanafunzi huyo hakurejea hadi usiku ndugu walihofia usalama wake na kuanza kumtafuta bila mafanikio kwa kuwa haikuwa tabia yake. Walikwenda hadi kwenye shamba ambalo aliaga anakwenda na hawakumpata,” alisema.
 
 Kwa mujibu wa Chande, Septemba 27, wanafamilia wakishirikiana na jamii walimtafuta maeneo mbalimbali na hawakumpata.
 
Alisema baada ya kumkosa kwa siku mbili, walitoa taarifa Serikali ya Mtaa na Kituo cha Polisi Wilaya ya Msasi.
 
Chande alisema ofisi ya serikali ya mtaa wa Mchema jana majira ya saa 9:00 jioni ilipata taarifa kutoka kwa wasamaria wema pamoja na wanafamilia kuwa mwili wa mwanafunzi huyo umeokotwa maeneo ya miamba ya milima ya eneo la Kabomola ukiwa umesokomezwa kwenye makorongo ya miamba hiyo.
 
Alisema kutokana na hali ya mwili kuharibika, ulizikwa siku hiyo hiyo majira ya saa 10 jioni.
 
Polisi mkoani humo ilithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba wanaendelea na uchunguzi.

Mkazi wa Mtaa wa Mchema, Ally Salvatory, alieleza kusikitishwa na tukio hilo la kikatili na kuiomba jamii kushirikiana kwa karibu.  Aidha, baadhi ya wakazi waliliomba Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi wa kina wa tukio hilo ili kukomesha matukio kama hayo.
 

Habari Kubwa