Mwanafunzi abambwa na bangi misokoto 50

16Jan 2019
Na Mwandishi Wetu
Moshi
Nipashe
Mwanafunzi abambwa na bangi misokoto 50

MWANAFUNZI wa kidato cha pili katika Shule ya Sekondari ya Kilingi, Siha mkoani Kilimanjaro, amekamatwa na polisi akiwa na misokoto  50 ya dawa za kulevya aina ya bangi.

Kwa sasa, mwanafunzi huyo anashikiliwa na Jeshi la Polisi katika Kituo Kikuu cha Polisi Sanya Juu kwa mahojiano ambayo yatawezesha kusaidia kukamatwa kwa mtandao wa watu wanaowatumia watoto kufanya biashara hiyo.

Taarifa za kukamatwa kwa mwanafunzi huyo, zilithibitishwa jana na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kilimanjaro, Hamisi Issah.

"Ni kweli huyo mwanafunzi alikamatwa jana (juzi) saa 12:30 jioni na anahojiwa. Ni mkazi wa Kijiji cha Majengo, Kata ya Sanya Juu, Wilaya ya Siha," alisema Issah.

Kamanda Issah alisema askari polisi wakiwa doria, walimkamata mwanafunzi huyo nyumbani kwao akiwa na misokoto hiyo ya bangi.

Katika tukio lingine lililotokea majira ya saa 1:00 jioni katika Kijiji cha Mabogini, wilayani Moshi, mtu mmoja aliyefahamika kwa jina moja la Jackson, mfugaji wa jamii ya Kimasai anayekadiriwa kuwa na umri kati ya miaka 40 hadi 45 ameokotwa akiwa ameuawa.

Kamanda Issah alisema mtu huyo ambaye ni mfanyabiashara wa dawa za asili za kimasai, aliuawa baada ya kushambuliwa na watu wasiofahamika huku mwili wake ukiwa na michubuko sehemu za miguuni na mgongoni.

Alisema mtu huyo hakuwa na makazi maalumu yanayofahamika na mara ya mwisho alionekana mitaani akiwa na mwenzake wa jamii ya Kimasai wakifanya biashara ya kuuza dawa mpaka alipokutwa akiwa amefariki dunia.

Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Rufani ya Mkoa ya Mawenzi huku Kamanda Issah akisema Jeshi la Polisi linaendelea kuwatafuta watuhumiwa wa tukio hilo.

Pia Kamanda Issah alisema tukio lingine lililotokea siku hiyo majira ya saa 1:30 jioni maeneo ya Kahe, Moshi, ambako Sadick Ally (45) mkazi wa Kahe, amekutwa amefariki dunia akiwa chumbani kwake huku mlango wa chumba hicho ukiwa umefungwa.

Habari Kubwa