Mwanafunzi adaiwa kujitoa ujauzito kwa kijiti

06May 2021
Marco Maduhu
SHINYANGA
Nipashe
Mwanafunzi adaiwa kujitoa ujauzito kwa kijiti

MWANAFUNZI anayesoma kidato cha kwanza katika Shule ya Sekondari Uzogole Manispaa ya Shinyanga (jina limehifadhiwa), amedaiwa kujitoa ujauzito kwa kijichokonoa na kijiti, ili aendelee na masomo.

Imeelezwa mwanafunzi huyo alipata ujauzito huo wakati akiwa nyumbani akisubiri matokeo ya kidato cha kwanza, na alipofaulu akaingia nao sekondari, ndipo Januari mwaka huu akaona autoe ili asifukuzwe shule.

Askari Polisi Kata wa Ibadakuli Manispaa ya Shinyanga ilipo shule hiyo, Emmanuel Maganjila, ilibainisha hayo juzi kwenye kikao cha kujadiliana kutokomeza matukio ya ukatili wa kijinsia kwenye kata hiyo, kilichoandaliwa na Shirika la YWCA.

Alisema mwanafunzi huyo alifanikiwa kujitoa ujauzito huo, na kwamba kilitoka kiumbe kikiwa kimekufa, lakini mwanafunzi huyo aliwahishwa hospitali kwa ajili ya matibabu, na sasa anaendelea na masomo.

"Natoa wito kwa wazazi mkoani Shinyanga vunjeni ukimya, zungumzeni na watoto wenu na kuwapatia elimu ya makuzi na madhara ya kufanya ngono katika umri mdogo," alisema Maganjila.

Naye Katibu wa Shirika la YWCA, Marysiana Makundi, ambao wanatekeleza mradi wa kutokomeza ukatili wa kijinsia kwenye Kata ya Ibadakuli, alisema matatizo hayo ya mimba za utotoni ili kuisha, inapaswa wahusika wawe wanafungwa jela badala ya kuachiwa huru.

Alisema mbali na utoaji wa elimu ya kutokomeza matukio ya ukatili wa kijinsia, wazazi wamekuwa kikwazo, kutokana na kuwa na tabia ya kumaliza kesi kimya kimya na watuhumiwa ambao huwapatia ujauzito wanafunzi, kwa kupeana fedha ama mifugo na kusababisha kesi kufutwa mahakamani kutokana na kukosekana ushahidi.

Ofisa Maendeleo ya Jamii wa Ibadakuli, Mwijage Patrick, aliwataka wazazi mkoani Shinyanga, waachane na mila kandamizi, ambazo zimekuwa zikimnyima haki mtoto wa kike, kwa kuonekana hastahili masomo bali ni wa kuolewa tu, na ndio chanzo cha mimba na ndoa za utotoni kuendelea kwa kasi mkoani humo.

Habari Kubwa