Mwanafunzi afa kwa ajinyonga kwa tai

22Feb 2021
Thobias Mwanakatwe
Songwe
Nipashe
Mwanafunzi afa kwa ajinyonga kwa tai

MWANAFUNZI wa kidato cha pili katika Shule ya Sekondari Ndugu wilayani Mbozi mkoani Songwe, Rehema Kapufi (15), amekufa kwa kujinyonga nyumbani kwa bibi yake, huku akiwa ameshika rozali mkononi.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, George Salala, akizungumza na gazeti hili, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo, na kwamba lilitokea Februari 13, mwaka huu majira ya saa 7:00 mchana katika kijiji cha Ilembo.

Salala alisema mwanafunzi huyo alijinyonga kwa kutumia tai mbili za kufunga shingoni, muda mfupi baada ya kurudi nyumbani kwa bibi yake akitokea shuleni.

Aidha, Kaimu Kamanda Salala alisema mwanafunzi huyo siku moja kabla ya kurudi nyumbani kwa bibi yake alikuwa ameadhibiwa shuleni kwao kwa tuhuma za kuiba begi.

“Kuna taarifa za awali zinaonyesha kabla ya mwanafunzi huyo kujinyonga, akiwa shuleni kwao, aliadhibiwa na walimu kwa tuhuma za wizi wa begi, hivyo tunaendelea kufuatilia ili kujua kama ndicho chanzo cha mwanafunzi huyo kuchukua uamuzi huo wa kujinyonga,” alisema Salala.

Hata hivyo, Kamanda Salala alisema katika mazingira ya mwanafunzi huyo kujinyonga, hakuna ujumbe wowote aliouacha.

 

Habari Kubwa