Mwanafunzi afariki kwa kichapo cha kufeli mtihani wa ‘Mock’

20Jul 2021
Gideon Mwakanosya
Songea
Nipashe
Mwanafunzi afariki kwa kichapo cha kufeli mtihani wa ‘Mock’

MWANAFUNZI wa Shule ya Sekondari wilayani Namtumbo, Mkoa wa Ruvuma mwenye umri wa miaka 15 (jina limehifadhiwa), amefariki dunia kwa madai ya kupewa adhabu ya kipigo na walimu wake baada ya kufanya vibaya mitihani ya Mock mkoa.

Mwanafunzi huyo ni miongoni mwa watu wengine watatu waliopoteza maisha wilayani humo katika matukio tofauti.

Kamanda wa Polisi mkoani Ruvuma, Joseph Konyo, akizungumza na waandishi wa habari jana ofisini kwake, alisema katika tukio la kwanza Jeshi la Polisi linafanya uchunguzi wa kifo cha mwanafunzi huyo ambaye inadaiwa Julai 18, mwaka huu majira ya saa 3:00 asubuhi katika kituo cha Polisi cha Namtumbo kilipokea taarifa za kifo chake.

Alisema inadaiwa katika taarifa hiyo mwanafunzi huyo alifariki wakati akipatiwa matibabu Kituo cha Afya cha Hanga baada ya kulazwa kutokana na majeraha ya kupewa adhabu ya kuchapwa viboko yeye pamoja na wanafunzi wenzake wa kidato cha kwanza na cha tatu.

Alisema inadaiwa Julai 19, mwaka huu, majira ya saa 5:00 asubuhi mwanafunzi huyo akiwa na wenzake walipewa adhabu na walimu wao kwa kufanya vibaya kwenye matokeo ya Mock mkoa walioufanya kabla ya kufungwa shule.

Alisema inadaiwa baada ya adhabu hiyo mwanafunzi huyo aliumia na kupata uvimbe kwenye paja la upande wa kulia pia katikati ya mgongo na ndipo wazazi wake walipompeleka Kituo cha Afya Hanga na siku ya pili majira ya saa 10:00 jioni mwanafunzi huyo alifariki dunia wakati akiendelea kupatiwa matibabu.

Kamanda Konyo alisema, walimu sita wa Shule ya Sekondari Mbunga wanashikiliwa na polisi kwa mahojiano zaidi.

Alilitaja tukio lingine la Julai 17, mwaka huu majira ya saa 7:00 mchana katika Kijiji cha Marungu, Kata ya Tingi, wilayani Nyasa, mwanaume mmoja mwenye umri wa miaka 85 (jina limehifadhiwa) mkazi wa Kijiji cha Marungu aliuawa baada ya kuvamiwa nyumbani kwake kisha kukatwa na shoka kichwani na mtu asiye fahamika.

Inadaiwa kabla ya tukio hilo mwanaume huyo alikuwa amelala nyumbani kwake na mkewe mwenye umri wa miaka 84.

Kamanda alisema, alikuja mtu na kuanza kugonga mlango kwa nguvu kama anabisha hodi bila kusema chochote ndipo mwanaume huyo alipolazimika kuamka na alipofungua mlango alivutwa nyuma ya nyumba yake na kuangushwa china kisha mtuhumiwa akaingia ndani na kuchukua shoka lililokuwa sebuleni ambalo alilitumia kumkata kichwani na kumsababishia kifo mzee huyo ambaye inadaiwa alikuwa akilalamikiwa kwa imani za kishirikiana. Polisi inaendelea kumsaka mtuhumiwa wa tukio hilo.

Katika tukio la tatu inadaiwa Julai 17, mwaka huu, majira ya saa 4:00 usiku katika Kijiji cha Lugali, Kata ya Mkumbi, wilayani Mbinga, mwanaume mwenye umri wa miaka 40 mkazi wa Kijiji cha Ngima wilayani humo, aliuawa na watu waliojichukulia sheria mkononi kwa kumkata miguu na mwili kwa kutumia kitu chenye ncha kali wakimtuhumu kuwa ni mwizi wa kuku.

Katika tukio hilo polisi inamshikilia mtuhumiwa mmoja na msako wa kuwakamata wahusika wengine unaendelea.

Pia, katika tukio lingine Julai 18, mwaka huu majira ya saa 2:00 usiku katika Kijiji cha Mtumbati Maji, Kata ya Mgombasi, mwanaume mmoja mwenye umri wa miaka 25, mkazi wa kijiji hicho alikutwa akiwa amefariki kwenye tembe la kuchomea tumbaku.

Alifafanua zaidi kuwa inadaiwa mwanaume huyo alikuwa ameenda shambani Julai 17, mwaka huu, kukagua maendeleo ya uunguaji wa tumbaku yake na alikuwa anaichoma na ndipo alipopatwa na ajali ya kuangukia kwenye shimo la tumbaku na kufia humo baada ya kuvuta hewa ya ukaa (carbon monoxide).

Kamanda Konyo alitoa rai kwa wananchi wanaojichukulia sheria mkononi kuacha mara moja.