Mwanafunzi ahukumiwa kifungo cha nje kwa kosa la kutoa mimba

09Dec 2021
Hadija Kitwana
Kilombero
Nipashe
Mwanafunzi ahukumiwa kifungo cha nje kwa kosa la kutoa mimba

MWANAFUNZI wa kidato cha tatu katika Shule ya Sekondari Nyandeo (jina linahifadhiwa), amehukumiwa kifungo cha nje mwaka mmoja baada ya kupatikana na kosa la kutoa mimba.

Hukumu hiyo ilitolewa juzi katika Mahakama ya Wilaya ya Kilombero mbele ya Hakimu Mkazi  Bestina Saning'o. 

Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Saning'o, alisema mahakama imesikiliza sababu za upande wa mashtaka baada ya kuomba kutolewa kwa adhabu kali kutokana na siku hizi vitendo vya utoaji mimba kushamiri katika jamii. 

Pia alisema amesikiliza upande wa mshtakiwa kuwa alishawishiwa na mtu aliyempa mimba na kwa kuwa mshtakiwa ameona bado ni mtoto wa miaka 16 na hakuisumbua mahakama, amemfunga kifungo cha nje.

Hakimu alisema kosa la kutoa mimba ni kinyume cha kifungu cha 151 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu Sura ya 16 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2019.

Alisema amemhukumu kifungo hicho kwa masharti mawili, la kwanza atakuwa chini ya uangalizi wa wazazi na la pili atakuwa chini ya ofisa ustawi wa jamii na atapangiwa kwenda kuripoti kwa ofisa huyo ili kuangalia tabia na mwenendo wake.

Kabla ya kusoma kwa hukumu, Mwendesha Mashtaka wa Jamhuri, Arnold Kiwoli, alidai kuwa shauri hilo lina washtakiwa wawili pamoja na mashtaka mawili.

Mshtakiwa wa kwanza katika  shauri hilo ni Winfrida Burton (21) mkazi wa Chikago A ambaye anashtakiwa kutoa dawa za kuwezesha kutoa mimba.

Alidai kuwa Novemba 8, mwaka huu, eneo la Chikago Kata ya Kidatu, Wilaya ya Kilombero, mshtakiwa alimpatia vidonge visivyojulikana binti huyo (jina linahifadhiwa) kwa lengo la kutoa mimba huku akijua binti huyo ni mjamzito.

Katika shtaka la pili, alidai linamkabili mwanafunzi kwa madai ya kutoa mimba na kwamba siku hiyo hiyo na maeneo hayo hayo, alimeza dawa zisizojulika ili kutekeleza kitendo hicho.

Mshtakiwa namba moja alikana kutenda kosa hilo, lakini mshtakiwa wa pili, alikiri kutenda kosa hilo na kujitetea kuwa alishawishiwa na kijana aliyempa mimba ambaye hakumtaja kwa jina bali alidai kuwa aliambiwa na kijana huyo aende kuchukua dawa hizo kwa Winifrida ili ameze na zisaidie kutoa mimba kwa kuwa yeye ni mwanafunzi ili aendelea na masomo.

Mahakama baada ya kutoa hukumu kwa mshtakiwa namba moja, iliahirisha kesi hadi Januari 10, mwakani, kwa ajili kusomewa maelezo ya awali.

Habari Kubwa