Mwanafunzi alivyokamatwa sare JWTZ

06Dec 2017
Romana Mallya
Nipashe
Mwanafunzi alivyokamatwa sare JWTZ

MWANAFUNZI wa Kidato cha Tatu wa Shule ya Sekondari Fahari, Goba jijini Dar es Salaam, Said Selemani (17), anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa madai ya kukutwa amevaa sare za Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).

Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salam, Lazaro Mambosasa

Selemani alishtukia akiwa kwenye sare hizo na wakati huo huo akiwa ndani ya benki huku akivuta sigara jambo ambalo si la kawaida. 

Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa, aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa mwanafunzi huyo alikamatwa maeneo ya Mbezi,  Benki ya CRDB huku akivuta sigara hadharani.

Alisema mwanafunzi huyo alikuwa akifanya vitendo vingine ambavyo haviendani na maadili ya askari aliyevaa sare. 

“Katika mahojiano ya awali, kijana huyu alijitambulisha ni askari toka kikosi cha 501 KJ kilichoko Lugalo jijini Dar es Salaam. Baada ya kubanwa zaidi alikiri kupata sare hizo toka kwa rafiki zake anaokuwa nao sehemu mbalimbali,” alisema Mambosasa. 

Aidha, alisema baada ya upekuzi kufanyika kwenye begi alilokuwa nalo,  alikutwa na kofia nyingine moja na kitambulisho namba DFF 7001A cha familia ya askari chenye namba 1231 ambacho ni cha mtoto wa askari wa JWTZ, Private Gabriel Kihwili wa 501 KJ kikiwa na picha ya mtoto wake, Elia Gabriel (4). 

Kamanda Mambosasa alisema uchunguzi wa tukio hilo unaendelea ili kuwapata rafiki zake hao ambao inadhaniwa huwa wanashirikiana katika kufanya matukio ya kihalifu. 

Katika hatua nyingine, jeshi hilo imeipata bajaji aina ya TVS yenye namba za usajili MC 473 BMM 5 rangi ya bluu iliyoibwa Oktoba 10, mwaka huu, Kigamboni Mjimwema nyumbani kwa Chandra Kandri.

Mambosasa alisema bajaji hiyo ilikamatwa Sumbawanga mkoani Rukwa ikiwa imetelekezwa na watu wasiojulikana, baada ya kushindwa kubadilisha umiliki wake.