Mwanafunzi apotea

24Nov 2022
Elizaberth Zaya
DAR ES SALAAM
Nipashe
Mwanafunzi apotea

JUNIOR Miller (14) mkazi wa Mbeya Mjini, mwanafunzi wa kidato cha tatu katika Shule ya Sekondari ya Airport mkoani humo amepotea.

JUNIOR Miller (14).

Kwa mujibu wa kaka wa mtoto huyo, Patrick Juma, mdogo wake huyo alipotea Novemba 20, mwaka huu, alipoaga kwenda kwenye masomo ya ziada ambayo huyapata katika shule hiyo ya sekondari.

Amesema wakati anaondoka nyumbani kwenda shuleni, alipewa fedha na baba yake Sh.150,000, ili akampatie mwalimu wake kwa ajili ya malipo ya masomo yake hayo ya ziada, lakini baada ya kupotea na familia yake kufuatilia walibaini kwamba hakupeleka fedha hizo kwa mwalimu.

“Mtoto aliondoka nyumbani saa tatu asubuhi na akapewa fedha kwenda kumpatia mwalimu wake kwa ajili ya kulipia masomo yake hayo ya ziada, lakini baada ya kufuatilia ikabainika kwamba hakupeleka japokuwa shuleni alifika na kuondoka kabla ya muda wa masomo kuisha,”amesema Patrick.

“Tumezungumza na rafiki yake ambaye anaishi Mwanjelwa, ametuambia kwamba siku hiyo hiyo alienda nyumbani kwao mchana akaazima baiskeli, wakampatia akaondoka, na ilipofika saa mbili ya usiku aliirejesha na kuwaambia kwamba anarudi nyumbani, lakini hakufanya hivyo mpaka hivi tunavyozungumza.”

Patrick ameeleza kuwa mdogo wake hajawahi kupotea kabla ya hapo.

“Tabia ya huyu mtoto ni njema tu na hatujawahi kusikia kwamba ana makundi mabaya na ndiyo maana tunapata shida kujua nini kimemkuta, tunaomba watakaomwona popote watusaidie, maana baada ya kukosekana kwake, tuliripoti kituo cha polisi na tukazunguka kila mahali ikiwamo hospitali bila mafanikio,”amesema Patrick.

Amesema mdogo wake wakati anaondoka nyumbani, alivalia suruali yenye rangi ya kijivu na shati ya drafti yenye rangi nyeupe na kijani pamoja na begi la shule lenye rangi ya bluu na kwamba rangi ya ngozi yake ni nyeusi na ni mwembamba, mrefu.

Ameomba kwa atakeyemwona awasiliane nao kwa namba 0767 626206, 0769906059 au atoe taarifa kituo chochote cha polisi.