Mwanafunzi aweka nia kuwania U-spika

14Jan 2022
Na Mwandishi Wetu
Arusha
Nipashe
Mwanafunzi aweka nia kuwania U-spika

MWANAFUNZI wa Shahada ya Uhasibu katika Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA), Juma Masende, ameweka nia ya kuwania nafasi ya uspika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambapo amesema kuwa uwezo wa kuongoza anao kutokana na nafasi mbalimbali ambazo amewahi kuongoza akiwa chuoni.

Juma Masende.

Akizungumza na waandishi wa habari mwanafunzi huyo amesema lazima achukue fomu ya kuwania nafasi hiyo ili aweze kuisaidia serikali katika kusimamia rasilimali za nchi pamoja na matumizi bora ya rasilimali.

“Mimi nataka kugombea hii nafasi kwani mimi ni kijana mdogo ambaye nina uchungu na nchi yangu na nataka kusimamia rasilimali za nchi yetu kikamilifu na kuhakikisha zinawanufaisha wananchi wake kwani uwezo wa kusimamia rasilimali ninao kutokana na uzoefu nilio nao kwa muda mrefu sasa.” amesema mwanafunzi huyo.

Amesema atasimamia kanuni ili kila Mtanzania aweze kunufaika na rasilimali za nchi pasipokuwepo upendeleo wowote kwani kiongozi anatakiwa kuwa muwazi na mzalendo ambapo wanategemea kupambania rasilimali ziliopo nchini kwa maslahi ya nchi.

Aidha, Masende amewaomba watanzania kumuunga mkono na kumwombea aweze kupata nafasi hiyo ya uspika kwani anataka kuwa kiongozi wa kuigwa na jamii na hata vijana wenzake ili waweze kutambua kuwa swala la kuwania uongozi ni la kila mmoja bila kujali umri kikubwa ni uwe na uwezo wa kuongoza nchi tu.

Habari Kubwa