Mwanamke apambana na jambazi kumwokoa mume

09Dec 2018
Na Mwandishi Wetu
Nipashe Jumapili
Mwanamke apambana na jambazi kumwokoa mume

MWANAMKE mkazi wa Kijiji cha Mahyolo, Bunda mkoani Mara, Busimba Malegesi, ameonyesha ushujaa wa aina yake baada ya kumwokoa mume wake baada ya kuvamiwa na jambazi mwenye silaha ambaye aliwaingilia usiku nyumbani kwao  wakiwa wamelala.

Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola (kulia), akimwangalia mgonjwa ambaye ni Mkazi wa Kijiji cha Mahyolo, Wilayani Bunda, Samson Malegesi aliyevamiwa na jambazi na kukatwakatwa mapanga mwili nzima, na kuokolewa na mkewe, Busimba Malegesi (katikati), kwa kumnyang’anya silaha jambazi na kulazwa katika Hospitali ya Kibara, Wilayani humo akiendelea kupewa matibabu. PICHA: WMN

Mtu huyo alipovamia nyumba hiyo kwa kuvunja mlango, alianza kumshambulia mume wa Busimba, Samson Malegesi (62) kwa kumkatakata mapanga mwili mzima.

Busimba alipoona hali hiyo, alimrukia jambazi huyo kiunoni na kumwangusha chini na  kumnyang’anya panga pamoja na tochi ambayo alikuwa nayo wakati anamshambulia mumewe.

Tukio hilo lilitokea saa 7:30 usiku wa kuamkia juzi wakati familia hiyo ikiwa imelala na ghafla walisikia mlango ukivunjwa na mtu huyo kwenda chumbani kwao kufanya tukio hilo.

“Baada ya kuingia aliwasha tochi na kuanza kumsaka Malegesi. Alipomwona alianza kumshambulia kwa kumcharanga mapanga kichwani, mikononi, kwenye mbavu na kusababisha damu nyingi kumwagika,” alisema.

Mwanamke huyo alisimulia kuwa wakati jambazi huyo akiendelea kumshambulia mume wake, alianza kupambana naye ili kumnusuru mume wake na hatimaye jambazi alizidiwa nguvu kwa kuangushwa chini na mwanamke huyo.

Busimba alisema wakati akipambana na jambazi huyo, alikuwa akipiga kelele lakini sauti yake haikuwafikia majirani ili kumpa msaada.

Hata hivyo, jambazi huyo alivyoona anakosa nguvu baada ya kukandamizwa chini na mwanamke huyo, alipata upenyo ndipo akakimbia kutoka katika nyumba hiyo.

Busimba alisema baada ya jambazi huyo kukimbia, alikwenda nje kuomba msaada zaidi kwa majirani ambao walifika na kumpeleka mume wake katika Hospitali ya Misheni ya Kibara wilayani Bunda.

Alisema mume wake alifikishwa hospitalini hapo akiwa hajitambui na kuanza kupatiwa matibabu ya haraka ili kuokoa maisha yake.

Muuguzi wa Hospitali hiyo, Godliver Josephat, alisema walimpokea mgonjwa huyo akiwa na wauguzi wenzake saa 9:00 usiku akiwa hajitambui.

Alisema alishirikiana na madaktari kumpatia matibabu ikiwamo kuzuia kutoka damu pamoja na kumwekea dawa za kusaidia kurudisha ufahamu wake.

“Tumempokea mgonjwa huyo akiwa kwenye hali mbaya. Jitihada zetu zilifanikiwa kumpa huduma ya kwanza kwa kumwekea dawa ya kumzindua na baadaye tukaendelea kumpa huduma zingine ikiwamo kuanza kumshona kwa sababu alikatwa panga la kichwa na mikono yake yote miwili ilijeruhiwa, “ alisema.

“Pia mbavu zake upande wa mgongoni zilichimbwa kwa kukatwa na panga, hivyo hali yake ilikuwa mbaya sana. Hata hivyo tumefanikiwa kumhudumia kwa umakini mkubwa na sasa mnamuona anaweza kuzungumza,” aliongeza muuguzi huyo alipokuwa akizungumza mbele ya Waziri wa mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola.

WAZIRI AMPONGEZA

Kutokana na kitendo alichokifanya, Waziri Lugola alimpongeza mwanamke huyo na kumuelezea kuwa ni shujaa.

“Nampongeza sana mwanamke aliyepambana na jambazi na kufanikiwa kumwokoa mume wake. Hakika kama si ushujaa wa mwanamke huyo, mume wake tungempoteza kwa sababu jambazi huyo alidhamiria kumuua kwa kumkata mapanga zile sehemu ambazo ni hatari zaidi kwa uhai wa ubinadamu,” alisema Lugola.

Waziri Lugola ambaye alikuwa katika ziara, baada ya kupata taarifa ya tukio hilo alfajiri ya jana, alifika hospitalini hapo kwa ajili ya kumjulia hali mgonjwa huyo.

“OCS (Mkuu wa Kituo cha Polisi) hakikisheni hamlali mpaka mnalipata hili jambazi kwa kutumia njia zote za kiintelejinsia mlizosomea ili kumkamata haraka iwezekanavyo. Huu ni unyama na lazima akamatwe. Mtafuteni usiku na mchana, msikae ofisini kunywa chai, hakikisheni huyu mtuhumiwa anakamatwa,” alisisitiza Lugola.

Waziri Lugola baada ya kutoa maelekezo hayo saa mbili asubuhi, alitoka hospitalini hapo na kuendelea na mikutano ya hadhara jimboni humo ambako alisisitiza kuwa majambazi wasiijaribu serikali.

Mkuu wa Kituo cha Polisi Kibara, Mwalupale alisema baada ya kupata taarifa ya tukio hilo, alipeleka askari kufanya msako mkali na alimhakikishia Waziri Lugola pamoja na wananchi kuwa watamkamata mtuhumiwa huyo.

“Jambazi huyo hakuiba chochote ndani ya nyumba hiyo. Hii inaonyesha kuwa lengo lake ilikuwa kuua tu. Sisi tunaendelea kufanya uchunguzi kujua lengo la mtuhumiwa huyo kufanya tukio hilo la kinyama na tutahakikisha tunamkamata na kumfikisha mahakamani,” alisema Mwalupale.

Habari Kubwa