Mwanasiasa Njelu Kasaka afariki dunia

04Jul 2020
Na Mwandishi Wetu
Mbeya
Nipashe
Mwanasiasa Njelu Kasaka afariki dunia

MWANASIASA mkongwe nchini aliyewahi kushika nyadhifa mbalimbali katika taasisi za umma na serikalini, Njelu Kasaka, amefariki dunia.

Njelu Kasaka:PICHA NA MTANDAO

Masache Kasaka, mtoto wa marehemu, aliliambia gazeti hili kwa simu kuwa Kasaka (78) alifariki dunia usiku wa kuamkia jana katika Hospitali ya Rufani ya Kanda, Mbeya alikokuwa anapatiwa matibabu. 

Kwa mujibu wa Masache, Kasaka alifikishwa hospitalini hapo kutoka Chunya baada ya kuugua ghafla Ijumaa iliyopita alipokuwa katika shughuli zake huko.

“Ni kweli baba amefariki (dunia) usiku wa kuamkia leo (jana) na hivi tunavyoongea msiba uko hapa nyumbani kwangu Mbeya mjini. Leo (jana) tunatarajia kusafirisha mwili wa mzee wetu kwenda nyumbani Chunya. Tunatarajia kumzika baba Jumapili (kesho),” alisema Masache.

Kasaka alikuwa Mbunge wa Chunya na baadaye Lupa kuanzia mwaka 1990 hadi 2005. Katika kipindi cha ubunge wake, Kasaka alijipatia sifa kutokana na kuongoza kundi la wabunge 55, maarufu kama G-55, ambalo liliibua vuguvugu la kudai serikali ya Tanganyika mwaka 1993.

Kabla ya kuwa mbunge, alikuwa mtumishi katika iliyokuwa Benki ya Maendeleo Vijijini (TRDB) ambayo ilibadilishwa na kuwa Benki ya Ushirika na Maendeleo Vijijini (CRDB) katika mikoa ya Kilimanjaro, Mtwara, Iringa na makao makuu, Dar es Salaam.

Katika kipindi cha ubunge, aliwahi kuwa Naibu Waziri wa Kilimo mwaka 1994 hadi 1996 kabla ya kuwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa na baadaye Tabora.

Sambamba na nafasi hizo, mwaka 2001 hadi 2005 alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Fedha na Mipango ambayo pamoja na mambo mengine ilisimama kidete katika ubinafsishaji wa Benki ya National Microfinance (NMB).

Kasaka ambaye ameacha mjane na watoto wanane, alizaliwa mwaka 1942 Chunya mkoani Mbeya. Alikuwa msomi katika fani ya uchumi ambapo alipata shahada ya kwanza ya uchumi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) mwanzoni mwa miaka ya 1970 na shahada ya pili katika Uchumi Kilimo aliipata Chuo Kikuu cha Kentucky, Marekani.            

Habari Kubwa