Mwandishi aachiwa kwa dhamana

15Mar 2019
Cynthia Mwilolezi
Arusha
Nipashe
Mwandishi aachiwa kwa dhamana

MWANDISHI wa habari  wa kujitegemea wa jijini Arusha,  Basil Elias, ameachiwa kwa dhamana na Jeshi la Polisi baada ya kushikiliwa tangu  juzi kutokana na kufuatilia malalamiko ya wananchi wanaougua matumbo na kuharisha.

Mkuu wa Mkoa Arusha, Mrisho Gambo, picha mtandao

Baadhi ya wakazi jijini hapa kwa nyakati tofauti, wamekuwa wakilalamika kuumwa homa za matumbo, kuharisha na kutapika kwa kile walichodai ni kutokana na kunywa maji yaliyochanganyika na maji taka.

Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira (Auwsa), ndiyo inayolalamikiwa lakini uongozi wa mamlaka hiyo ulitoa taarifa ya kukanusha kuwepo kwa maji yaliyochanganyika na maji taka (kinyesi).

Kuachiwa kwa mwandishi huyo kumetokana na waandishi wa habari mkoani hapa kwenda kwa Ofisi za Kamanda wa Polisi wa Mkoa huo mapema asubuhi jana, kuomba aachiwe kwa kuwa alikamatwa wakati akitekeleza majukumu yake ya kazi.

Akizungumza mara baada ya kuachiwa, Elias alisema kabla ya kukamatwa Machi 13, majira ya saa 11:00 jioni, alipigiwa simu na mwananchi aliyejitambulisha kwa jina la Anna Nathaniel, Mkazi wa Engutoto jijini hapa na kutoa malalamiko yake ya kutiririshiwa maji taka kwenye bomba lake la Auwsa.

Alisema baada ya kupata taarifa hizo ikiwa mara ya pili kujirudia kitu hicho kwake, aliwasiliana na Katibu Tawala wa Mkoa (RAS) na kuelekezwa kwenda kwa Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Gabriel Daqarro, ambaye naye alimpatia wataalamu wa kwenda nao eneo la tukio kujiridhishisha na taarifa hizo.

“Tuliongozana hadi kwa mama huyu na tulipofika tukaona kweli kuna hilo tatizo, wataalamu waliamua kutoa maji machafu kwenye chemba za majirani zake, wakidhani labda yanaingia kwake na walipoyatoa bado wakaona yanaendelea kutoka wakadhani mtandao wa Auwsa umepasuka mahali na kuingia kwake, ikabidi nimpigie Mkurugenzi wa Auwsa kumweleza suala hili,” alisema.

Alisema baada ya kumaliza kuona hali halisi waliondoka na kurudi mjini, lakini wakiwa njiani mmoja wa wataalamu hao walimweleza  amepokea simu toka kwa Mkurugenzi wa Auwsa kuwa wampeleke kituo cha polisi kwa kutoa taarifa za uchochezi.

“Nilipelekwa moja kwa moja polisi saa 11:00 jioni na nilipofika nikawekwa ndani na nikalala hadi leo (jana) hii ninavyoachiwa kwa dhamana na maelezo waliyochukua ya tukio la mimi kufuatilia taarifa ya maji machafu na sijahojiwa kitu kingine chochote na sijafanya kitu chochote,” alisema.

Mapema jana asubuhi, waandishi wa habari walikusanyika ofisi za Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha kumsubiri ili kufahamu hatima ya mwenzao. Walipofika walipata taarifa Kamanda yuko kwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha ana kikao na ndipo walipoamua kumfuata huko.

Akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na sakata hilo katika kikao ofisini kwake,  Mkuu wa Mkoa Arusha, Mrisho Gambo, alisema kushikiliwa kwa mwanahabari huyo kumetokana na makosa mengine na si suala la kufuatalia maji machafu yanayodaiwa na watu.

“Lakini msifikiri kuja kwenu kwa wingi hapa mnatutisha sisi serikali tusifanye kazi zetu hapa. Nilimwagiza RPC amwachie kwa dhamana jana (juzi), japo ana makosa mengine aliyofanya na si lazima tuwaeleze nyie mtaharibu upelelezi,” alisema.

Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Arusha, Claud Gwandu, alilaani kukamatwa kwa mwandishi huyo na kumwomba Mkuu wa Mkoa kama kuna tatizo washirikishane kabla ya kuchukua uamuzi wa kukamatana sehemu ya kazi.

“Tena kibaya mkuu tulipofuatilia jana kwa RPC alituambia amepokea maagizo toka juu yaani kwako wewe. Sasa hii inakuwaje?” alihoji.
Alisema chama hakitetei  uovu lakini kukamata watu wakiwa kazini ni sawa na kutisha waandishi wasifanye kazi zao kwa misingi ya sheria na kuwataka waandishi kutoogopa bali waendelee kufanya kazi zao kwa kuzingatia sheria za kazi.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Jonathan Shana, akizungumza katika kikao hicho, aliwaambia waandishi wa habari kuwa ameshatoa maelekezo ya kuachiwa kwa dhamana mwandishi huyo.

“Kweli Mkuu wa Mkoa jana uliniambia tumwachie kwa dhamana lakini tulikuwa bado hatujamalizana naye mahojiano na leo (jana) hii nimeshaagiza apewe dhamana,” alisema.

Zaidi ya wiki moja sasa baadhi ya maeneo ya Arusha kumekuwa na malalamiko ya wananchi kuhara, kuugua matumbo na kutapika kwa madai ya kunywa maji ya Auwsa ambayo yameingiliana na maji taka, madai ambayo Auwsa wanayakanusha kuwa maji hayo ni safi na salama.