Mwandishi The Guardian Limited ang’ara Tuzo FEMNET

14Oct 2021
Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM
Nipashe
Mwandishi The Guardian Limited ang’ara Tuzo FEMNET

MWANDISHI wa habari wa magazeti ya The Guardian na Nipashe, Jenifer Gilla, ameshinda Tuzo ya Usawa wa Kijinsia, kipengele cha mazingira, zinazotolewa na Shirika la The African Development and Communication (FEMNET).

Tuzo hizo zilitolewa jana mjini Nairobi nchini Kenya, katika hafla ya Mkutano Mkuu wa nane wa FEMNET wa kutetea haki za wanawake.

Tuzo hizo zilitolewa katika makundi matano ya kuzuia ukatili dhidi ya wanawake na mabinti likiwamo la mazingira, uongozi wa wanawake wenye mabadiliko, haki ya kiuchumi na haki ya afya ya uzazi.

Katika mashindano hayo jumla ya wanahabari 389 kutoka nchi 17 za Afrika na kati yao 15 walishinda katika mashindano hayo katika nafasi ya kwanza, pili na tatu.

Mratibu wa mkutano huo, kutoka FEMNET, Rachel Kagoiya, akizungumza kuhusiana na mkutano huo, alisema ulifanyika kwa siku mbili kuanzia Oktoba 12 hadi 14 na jumla ya washiriki 100 walikutana na wengine kwa njia ya mtandao kutokana na janga la UVIKO-19.

“Nafikiri wanachama kutoka Tanzania kikiwamo Chama cha Wanahabari Wanawake (TAMWA), wamefanya kazi ya kutetea haki za wanawake na wasichana kwa miaka 12 sasa,” alisema.

Alisema walitoa tuzo hizo kwa mara ya kwanza ili kuwatambua waandishi wa habari wanaofanya kazi nzuri ya kuandika changamoto za wanawake.

Alisema mkutano huo ulitambulika kwa jina la Wanawake wa Kiafrika, Jinsia na Wanaharakati wa Haki za Wanawake wa Pan-African.