Mwandishi IPP ashinda tuzo ya afya kimataifa

13Jan 2022
Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM
Nipashe
Mwandishi IPP ashinda tuzo ya afya kimataifa

SHIRIKA la Merck Foundation la Ujerumani kwa kushirikiana na wake wa marais wa Afrika, limemtangaza mwandishi wa habari wa magazeti ya The Guardian na Nipashe, Christina Mwakangale, kuwa  mshindi wa kwanza wa Tuzo ya Afya ya Uzazi Mwaka 2021 kwa nchi za Afrika Mashariki.

Christina Mwakangale.

Mbali na Mwakangale, Watanzania wengine walioshinda nafasi ya kwanza kwenye tuzo hiyo mtandaoni ni Veronica Mrema, kutoka blog ya matukio na maisha pamoja na Adam Gabriel Hhando, wa CG FM , kipengele cha redio.

Shirika hilo lilitangaza kuanza kwa mashindano hayo mwaka jana na kushirikisha nchi tofauti barani Afrika kutoka kanda mbalimbali kuwania tuzo kwa waandishi wa habari kutoka nchi za Kusini mwa Afrika; Afrika Mashariki; Afrika Magharibi na zinazozungumza lugha ya Kifaransa.

Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo, Seneta Dk. Rasha Kelej, akitangaza majina ya washindi hao kwenye taarifa yake jana, alisema lengo la mashindano hayo ni kukuza uelewa na kutoa elimu kwa jamii kuachana na dhana potofu dhidi ya watu waliokosa watoto, wakiwamo wagumba na tasa.

Mkurugenzi huyo ambaye pia ni rais wa shirika hilo linaloshirikiana na wake wa marais wa barani Afrika, alisema tuzo hizo hutolewa kila mwaka kwa kuhusisha waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali vya habari.

“Kaulimbiu ya tuzo hizo ilikuwa kukuza uelewa kuhusu kinga ya ugumba, kuvunja unyanyapaa na kuwawezesha wasichana na wanawake kupata elimu. Ninayo furaha kuwatangaza washindi hawa wa Merck Foundation Africa Media Recognition Awards ‘More Than a Mother’ 2021.

“Pia nachukua fursa hii kuwashukuru marais wa Afrika kwa nia yao thabiti na kushirikiana na shirika kama mabalozi wa Merck Foundation Zaidi ya Mama. Ninapongeza vyombo vya habari barani Afrika ambavyo vimekuwa sauti ya wasio na sauti na kuongeza uelewa kwenye jamii hususan unyanyapaa kwa wagumba, tasa na wanaopitia changamoto za kupata watoto,” alisema Dk. Kelej.

Pia alibainisha kwamba kila mara jukumu kuu la vyombo vya habari vina uwezo wa kuleta mabadiliko ya kitamaduni katika jamii zetu kwa njia ya gharama nafuu.

“Ninawakaribisha washindi wote kuwa wanachama wa walimu wetu wa Merck Foundation na kufanya kazi kwa karibu nasi, ili kuunga mkono, kuwawezesha wanawake na wasichana katika ngazi zote.

“Nimefurahishwa sana na kazi iliyoonyeshwa na washindi wetu wote; kwa hivyo inanipa furaha kubwa kutangaza kwamba Merck Foundation pia inawazawadia washindi kwa kuwapa ufikiaji wa mwaka mmoja wa programu ya MasterClass,” alisema.

Alisema kozi hiyo itawajengea washindi hao uzoefu wa kipekee wa mtandaoni na kujifunza ya haraka ambayo hufikiwa popote kwa njia ya mtandao.

"Ningependa pia kutoa wito wa Maombi kwa Merck Foundation Africa Media Recognition Awards 'Zaidi ya Mama' kwa mwaka 2022.”

Habari Kubwa