Mwandishi MCL apigwa akitekeleza majaukumu yake Zanzibar

21Apr 2021
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Mwandishi MCL apigwa akitekeleza majaukumu yake Zanzibar

Mwandishi wa habari, Jesse Mikofu, ameshambuliwa na askari wa vikosi vya SMZ wakati akitekeleza majukumu yake ya kazi leo asubuhi Jumatano Aprili 21, 2021.

Mwandishi huyo ambaye ni wa kampuni ya Mwananchi Communications Ltd (MCL) Zanzibar, kupitia taarifa yao ambayo Guardian Digital imeiona imeeleza kupigwa kwa Mikofu.

Mikofu amekumbwa na kadhia hiyo baada ya kuwapiga picha askari hao wakati wakitekeleza jukumu lao la kuwahamisha wamachinga waliopanga bidhaa zao barabarani katika eneo la darajani.

Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Awadh Juma Haji amesema hana taarifa za tukio hilo na kuahidi kutoa ushirikiano zitakapomfikia.

Akisimulia hali ilivyokuwa, Mikofu amesema pamoja na kupigwa, kuvutwa, kutakiwa kugaragara kwenye maji machafu na kupiga push-up, vifaa vyake vya kazi ikiwemo simu ya mkononi aliyoitumia kupiga picha vimeharibiwa.

“Nilifika darajani na kukuta askari wanabeba meza zilizokuwa zikitumiwa na wamachinga na kuzipandisha kwenye magari yao, nikatoa simu na kuanza kupiga picha, nyuma yangu wakatokea askari wakanihoji nikajitambulisha na kuonyesha vitambulisho.”

“Hawakuridhishwa wakanipeleka kwa kiongozi wao ambako huko ndiko nilikokutana na adhabu, niliambiwa nikae chini ninyooshe miguu, nipakate mawe makubwa wakiniambia niyabembeleze kama mtoto,” amesema.

Pamoja na adhabu hiyo Mikofu aliendelea kupigwa na askari hao wakimtaka kuonyesha picha alizopiga na baadaye kumlazimisha kubadili nywila kwenye barua pepe yake.

“Kiongozi wao akaandika namba yake kwenye simu yangu ili nimtumie zile picha nikazituma, wakaniambia nibadilishe passwords (nywila) nikagoma, akaitwa askari mwingine akabadilisha palepale, kisha wakanilazimisha niipige ile simu kwenye mawe hadi ivunjike, sikuwa na namna nyingine nikafanya hivyo,” amesisitiza.

Amesema pia akaelekezwa kuingia kwenye dimbwi la maji ya mvua yaliyotuama na kugaragara kwenye maji hayo na baada ya kitendo hicho aliruhusiwa kuondoka katika eneo hilo.

Habari Kubwa