Mwanjelwa awataka watumishi wa umma kutotumika kisiasa

26Feb 2019
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Mwanjelwa awataka watumishi wa umma kutotumika kisiasa

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa amewataka watumishi wa umma nchini kutotumika kisiasa kwani uwepo wao una lengo mahususi la kuboresha utoaji huduma-

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa.

wenye viwango stahiki ikiwa ni pamoja na kuijenga Serikali ili iweze kuleta maendeleo kwa wananchi.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri huyo wakati wa kikao kazi na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe chenye lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi hao, kabla ya kutembelea wanufaika wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini wilayani Kisarawe ili  kujiridhisha na utekelezaji wa mpango huo. Mhe. Dkt. Mwanjelwa amesema, serikali inahitaji utaalam wa watumishi wa umma katika kujenga utumishi wa umma imara uliotukuka, utumishi ambao utaziwezesha taasisi za umma zote nchini kutoa huduma stahiki kwa wananchi. 

Mhe. Dkt. Mwanjelwa amesisitiza kuwa, hategemei kumuona mtumishi wa umma yeyote akijihusisha na siasa zinazosababisha kukwamisha azma ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kuwahudumia wananchi wake kikamilifu.

Aidha, Mhe. Dkt. Mwanjelwa amewataka Makatibu Tawala wa Mikoa kuwasimamia kikamilifu Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri ili kujenga ushirikiano wa kiutendaji kati ya Makatibu Tawala wa Wilaya  na Wakuu wa Wilaya kwa lengo la kuboresha utoaji huduma bora kwa umma.  

Habari Kubwa