Mwanza kupokea bilioni 24.3 kupunguza umaskini

24Apr 2022
Neema Emmanuel
MWANZA
Nipashe Jumapili
Mwanza kupokea bilioni 24.3 kupunguza umaskini

MKOA wa Mwanza unatarajia kupokea kiasi cha zaidi ya Sh. bilioni 24.3 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya kupunguza umaskini.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhandisi Robert Gabriel.

Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhandisi Robert Gabriel,wakati akifungua kikao kazi cha kujengeana uelewa wa pamoja kuhusu utekelezaji wa miradi ya kupunguza umaskini awamu ya nne(TPRP IV) katika mpango wa TASAF Mkoa wa Mwanza.

Amesema kati ya miradi hiyo 23 ni miradi ya ujenzi wa miundombinu ya elimu,miradi ya afya 16 pamoja na mradi wa ajira za muda 1 hivyo viongozi wote wanapaswa kuzingatia sheria,kanuni, taratibu na miongozo wakati wa utekelezaji wa miradi hiyo pamoja na usimamizi thabiti ili thamani ya fedha itakayotumika iendane na ubora wa miradi hiyo.

Pia ameongeza kuwa katika  mwaka wa fedha wa 2021/2022 Mkoa wa Mwanza umepokea kiasi cha zaidi ya Sh. bilioni 3.2 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi 40 ikiwemo ya ujenzi wa miundombinu ya elimu,afya na ajira za muda.

Aidha Mratibu wa TASAF Mkoa wa Mwanza, Monica Mahundi, amesema Mkoa wa Mwanza ni miongoni mwa mikoa mitano inayotekeleza miradi ya kupunguza umaskini awamu ya nne ambapo wamepokea  zaidi ya bilioni 3.2 ya kutekeleza miradi 40 na kila Halmashauri ikitekeleza miradi mitano.

"Kama Mkoa tumejipanga  kutekeleza miradi hiyo ipasavyo na kwa ufanisi na kufuata maelekezo na taratibu zilizotolewa." ameeleza Mahundi.

Kwa upande wake Katibu Tawala Masidizi- Mipango na Uratibu Mkoa wa Mwanza, Joachim Otaru, amesema zoezi la uibuaji wa miradi ya kupunguza umaskini awamu ya nne(TPRP IV), jumla ya miradi 104 imeibuliwa na kupitishwa na Wizara kwa ajili ya utekelezaji kati ya miradi hiyo 31 ni ya afya,49 elimu na 24 ni miradi ya kutoa ajira za muda(PWP),jumla miradi hiyo itagharimu kiasi cha zaidi ya Sh. bilioni 7.8.

Pia amesema,mafanikio yaliyopatikana  katika utekelezaji wa TASAF awamu ya tatu ni pamoja na kuwa na ongezeko  la mahudhurio  ya wanafunzi shuleni na kwa watoto wenye umri wa kuhudhuria huduma ya kliniki  kwa asilimia 95.

Kwa kuzingatia ruzuku inavyotolewa kwa kutimiza masharti ya kuhudhuria shule na kliniki ambapo jumla ya watoto 39,567 wametimiza masharti ya elimu na afya. 

Habari Kubwa