Mwekezaji akana kulima bangi

25Feb 2021
Godfrey Mushi
Moshi
Nipashe
Mwekezaji akana kulima bangi

MWEKEZAJI raia wa Poland, Damian Jankowski, ambaye anakabiliwa na kesi ya ulimaji wa dawa za kulevya aina ya bangi na kufanya mauzo ndani na nje ya nchi, amedai kuwa eneo analodaiwa kulima bangi ya kisasa miche 729, alikuwa ameotesha michikichi.

Pia amedai siku ambayo alipelekwa Kituo Kikuu cha Polisi Moshi, polisi walimpa makaratasi atie saini na walipoona haelewi na anasita kutia saini, walimtishia kwa bastola.

Jankowski na wenzake watatu ambao ni mkewe Eliwaza Pyuza, mfanyabiashara Hanif Kanani na Boniface Kessy, wanakabiliwa na mashtaka manne ya kulima bangi, matumizi ya bangi, kufanya mauzo na kusafirisha bangi.

Akiongozwa kutoa ushahidi wake jana na Wakili wa Utetezi Faygrace Sadala, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi, Jankowski alidai kwamba yeye havuti bangi, isipokuwa kuna uwezekano akawa amepata athari ya dawa hizo kwa kuwa alikaa karibu na moto uliochoma maua yanayodaiwa kuwa ni bangi.

Kesi hiyo namba 79 ya mwaka 2020, inasikilizwa na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Bernazitha Maziku.
Katika ushahidi wake, Jankowski alidai kuwa baada ya kujenga ukuta kwenye eneo la Nji Panda ya Himo, alilomnunulia mwanawe wa kike, Maryssa, kwa ajili ya kumjengea nyumba, alikuwa ameotesha michikichi.

Aliendelea kudai kuwa maua aliyoyaotesha katika eneo hilo yalikuwa na ukubwa wa robo hekari.

“Sijawahi kuwa na bangi nyumbani, mke wangu (Eliwaza) hajui chochote kuhusu bangi na siku ya Februari 9, 2020, ndiyo mara ya kwanza kuona hayo maua pale Himo.

“Baada ya kufika Himo, Polisi walituambia tung’oe na tuyasambaze hayo maua na baada ya hapo wakaangalia uzito wa hayo maua yakiwa na mizizi yake na udongo na kuyachoma,” alidai.

Alipoulizwa na Wakili wa Serikali, Ignas Mwinuka, wakati wa mahojiano kwamba asali iliyokamatwa nyumbani kwake kama ndiyo ile iliyoonyeshwa mahakamani, shahidi huyo alikiri ndiyo halisi na alikuwa anaitumia na familia yake kwenye chai, badala ya sukari.

Februari 17, mwaka huu, Mahakama hiyo ilimwona Jankowski na wenzake watatu ambao ni raia wa Tanzania, wana kesi ya kujibu katika mashtaka hayo.

Hakimu Maziku aliwaona wana kesi ya kujibu baada ya upande wa mashtaka kufunga ushahidi wa mashahidi wa upande wa mashtaka.

Upande wa mashtaka ukiongozwa na mawakili wa serikali kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka (NPS), Ignas Mwinuka na Verdiana Mlenza, ulifunga ushahidi wake baada ya mashahidi 11 kutoa ushahidi wao pamoja na kuwasilisha vielelezo 36.

Katika hati ya mashtaka, washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka manne ambayo ni kulima dawa za kulevya kinyume na kifungu cha 11 (1) (a) cha Sheria ya Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, Namba 5 ya Mwaka 2015.

Mshtakiwa wa kwanza, pili na wa tatu wote kwa pamoja wanadaiwa kuwa Februari 8, mwaka jana, huko katika eneo la Njia Panda ya Himo, Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro, walikutwa wamelima miche ya bangi 729.

Wakati kosa la pili ambalo linawakabili mshtakiwa wa kwanza, pili na wa tatu, ni kusafirisha bangi kinyume na kifungu cha 15A (1) (2) (C) cha Sheria ya Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, Namba 15 ya Mwaka 2017 kama ilivyofanyiwa marejeo.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, washtakiwa hao pia wanadaiwa kukutwa na kilogramu 15.6 za bangi katika eneo la Shirimatunda, Manispaa ya Moshi, Februari 8, mwaka jana.

Kosa la tatu ni kusafirisha dawa za kulevya kinyume na kifungu cha 15A (1) (2) (C) cha Sheria ya Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, Namba 5 ya Mwaka 2015 kama ilivyofanyiwa marejeo kifungu cha 9 cha Sheria ya Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, Namba 15 ya Mwaka 2017.

Na kosa la nne ni matumizi ya dawa za kulevya, kinyume na kifungu cha 18 (a) cha Sheria ya Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, Namba 5 ya Mwaka 2015. Kesi hiyo itaendelea tena leo mahakamani hapo.

Habari Kubwa