Mweli awataka ma-RAS,DED kuanzisha mtandao kubadilishana uzoefu kazini

16May 2021
Na Mwandishi Wetu
Dodoma
Nipashe Jumapili
Mweli awataka ma-RAS,DED kuanzisha mtandao kubadilishana uzoefu kazini

​​​​​​​NAIBU Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa,Gerald Mweli, amewataka Makatibu Tawala wa Mikoa na Wakurugenzi kuanzisha mtandao kwa ajili ya kujifunza na kubadilishana uzoefu katika utekelezaji wa Miradi ya maendeleo.

Gerald Mweli.

Mweli ametoa agizo hilo leo Mei 16,2021 wakati akifungua Mkutano wa 11 wa Umoja wa Makatibu Tawala wa Mikoa na Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa (TOA), unaofanyika kwa siku tatu Jijini Dodoma huku kauli mbiu yake ni mipango na bajeti inayozingatia huduma endelevu za jamii.

Mweli amesema kwa sasa kumekuwa na changamoto kubwa ya kusuasua kwa utekelezaji wa miradi katika baadhi ya Halmashauri pamoja na Serikali kutoa fedha kwa pamoja na kwa wakati

“Kuna baadhi ya Halmashauri zimepelekewa fedha za ujenzi wa mabweni shilingi milioni 80, kuna wengine wamemaliza na kuweka na vitanda lakini wengine bado. Hata pale serikali inapotoa fedha za ujenzi wa madarasa Halmashauri mmoja inaweza kuona shilingi milioni 20 zilizotolewa hazitoshi lakini kuna wengine kwa kiasi hicho hicho wanamaliza na madawati ndani, sasa kutumia mkianzisha mtandao huo itakuwa rahisi kushirikisha wenzako uzoefu huo ili nao waweze kamilishe mradi huo” amesema Mweli.

Ameendelea kufafanua kuwa uanzishwaji wa mtandao wa kujifunzia kutasaidia kujifunza changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika Halmashauri hasa katika suala zima la utekelezaji wa miradi ya maendeleo nchini.

Aidha Mweli amewataka watendaji hao kutumia mtandao huo kubadilishana uzoefu kuhusu njia mbora ya utekeleza miradi ya maendeleo katika maeneo yao kwa kutumia mfumo wa force akaunti na kwa kutumia mkandarasi.

Habari Kubwa