Mwenge waipa kongole NCA na 4CCP miradi ya maji vijijini

15Jun 2019
Godfrey Mushi
Mbulu
Nipashe
Mwenge waipa kongole NCA na 4CCP miradi ya maji vijijini

UBORA wa visima virefu vinavyochimbwa kwa ufadhili wa Shirika la Misaada la Makanisa ya Norway (NCA) na Kituo cha Utamaduni cha 4CCP katika vijiji vinavyokabiliwa na ukame eneo la Mbulu Vijijini, umemfurahisha Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa, Mzee Mkongea Alli.

Mratibu wa Kituo cha Utamaduni cha 4CCP, Eliminata Awet .

Kiongozi huyo ameeleza imani yake aliyonayo katika miradi hiyo, akisema kuna kila sababu ya wadau wengine wa maendeleo kuiga mfano wa kazi na misaada yenye tija kwa watanzania.

Alikuwa akizungumza leo katika Kijiji cha Getanyamba, Mbulu Vijijini, wakati akizindua mradi wa maji wa kisima kirefu utakaohudumia zaidi ya wananchi 1,000.

Kabla ya kiongozi huyo wa mbio za mwenge wa uhuru kitaifa kuzindua mradi huo, Mkuu wa Wilaya ya Mbulu, Chelestino Mofuga alimweleza Alli kwamba mradi huo utawawezesha wananchi wa Getanyamba iliyopo Kata ya Geterere, Tarafa ya Hydom kupata majisafi na salama kwa karibu na kupata muda wa kutosha kufanya shughuli nyingine za maendeleo.

"Idadi ya watu waliopo katika kijiji hiki ni 4,250 na wakazi wanaohudumiwa na mradi huu ni zaidi ya 1,000 ambao ni sawa na asilimia 24 ya wakazi wote,"alisema Mofuga.

Licha ya mradi huo kupeleka ahueni kwa wananchi hao, bado kuna wananchi wengine 3,250 hawajafikiwa na huduma ya majisafi na salama.

Akitoa ufafanuzi zaidi kuhusiana na utekelezaji wa mradi huo, Mratibu wa Kituo cha Utamaduni cha 4CCP, Eliminata Awet alisema kabla ya kujengwa mradi huo wananchi hao walikuwa wakitembea umbali mrefu wa kilomita 3 hadi 5 kwa siku kwenye korongo la Hydom na Kijiji cha Endagaw.

"Mradi huu ulianza kujengwa Septemba mosi mwaka 2017 kwa kuchimba kisima kirefu cha maji chenye urefu wa mita 100 na kufungwa pampu ya mkono lakini mwezi Oktoba mwaka 2018, mradi uliboreshwa zaidi kwa kuwekewa miundo mbinu ya kusukuma maji kwa kutumia nishati ya jua,"ameeleza Awet

Kwa mujibu wa mratibu huyo, mradi huo umegharimu zaidi ya Sh.milioni 61.9 hadi kukamilika kwake.

Habari Kubwa