Mwenye asili ya Tanzania aweka historia Pakistan

16Aug 2018
Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM
Nipashe
Mwenye asili ya Tanzania aweka historia Pakistan

MWANAMAMA Tanzeela Qambrani, aliye na asili ya Tanzania amekuwa wa kwanza wa asili ya Afrika kuteuliwa kuwa mbunge nchini Pakistan, na kutoa matumaini kwa watu wa jamii ndogo na maskini nchini humo yenye asili ya Afrika.

MWANAMAMA Tanzeela Qambrani, akipongezwa na baadhi ya wanawake wa jimbo hilo.

Tanzeela mwenye miaka 39, aliteuliwa na chama cha Pakistan People's Party (PPP), cha waziri wa zamani,  Benazir Bhutto kuhudumu katika kiti kilichotengewa wanawake kwenye bunge la mkoa wa Sindh kusini mwa India.

Alisema ana matumaini kuwa uteuzi wake baada ya uchaguzi wa mwezi uliopita utasaidia kuondoa unyanyapaa ambao umekuwepo dhidi ya jamii ya Sidi, jina wanaloitwa watu wa asili ya Afrika wanaoishi maeneo ya pwani ya Makran na Sindh nchini Pakistan.

"Kama jamii ndogo iliyopotelea kwenye jamii kubwa za wenyeji, tumekuwa na wakati mgumu kudumisha mizizi yetu ya Afrika na tamaduni, lakini ningependa kuona kuwa jina Sidi linakuwa lenye heshima," Qambrani ambaye mababu zake walitokea Tanzania aliiambia BBC.

 

Mwanamke huyo aliapishwa Jumatatu wiki hii na amenukuliwa na mtandao wa The News International akisema kwamba alijihisi kama Nelson Mandela.

Katika jitihada za kuenzi asili yake alivalia mavazi ya kitamaduni ya Kiafrika wakati wa kuapishwa kwake.

Watu wengi wa jamii ya Sidi walitokana na watumwa waliopelekwa India kutoka Afrika Mashariki na Wareno.

Wanahistoria wanasema mababu zao walikuwa pia wanajeshi, wafanyabiashara, madereva na mahujaji wa Kiislamu.

Walishika nyadhifa za juu wakati wa utawala wa Mughal lakini wakatengwa sana chini ya ukoloni wa Mwingereza.

Makadirio yanaonyesha kuwa idadi yao ni elfu kadha nchini Pakistan.Walichanganyika na watu wengine lakini wao wamedumisha baadhi ya tamaduni zao.

Wanajamii hao wanaandaa tamasha ambalo huchanganya baadhi ya imani za Kiislamu na mamba, na pia nyimbo zao huchanganya Uswahili na lugha ya wenyeji ifahamikayo kama Baluchi.

Jamii za Sidi pia huishi kwenye majimbo ya Karnataka, Gujarat na Andhra Pradesh nchini India.

Watu wa jamii ya Sidi ni wengi wilaya ya Lyari huko Karachi na wamekuwa wafuasi wakubwa wa chama cha PPP ambacho kwa sasa kinaongozwa na mtoto wake Benazir Bhutto, Bilawal Zardari Bhutto.

Hata hivyo, hakuna mtu kutoka jamii ya Sidi aliwahi kuingia bungeni hadi Bhutto Zardari alipomteua Qambrani kwenye kiti maalum.

"Kama vile Colombus alivyogundua Amerika, Bilawal (mwanawe Benazir Bhutto) pia amewagundua watu wa jamii ya Sidi," alisema Qambrani ambaye mababu zake waliingia Sidhi wakitokea Tanzania.

Chama cha PPP kilichukua nafasi ya tatu kwenye uchaguzi uliopita, kilishuhudia ushindi wa mcheza kriketi wa zamani Imran Khan wa chama cha PTI, akiibuka kidedea.

Mbunge mteule Qambrani ni mtaalamu wa ya kompyuta na ana shahada ya uzamili (shahada ya pili) kutoka Chuo Kikuu cha Sindh, Jamshoro.

BBC Swahili

Habari Kubwa