Mwenyekiti Bunge akalia kuti kavu

13Jun 2018
Na Mwandishi Wetu
DODOMA
Nipashe
Mwenyekiti Bunge akalia kuti kavu

MWENYEKITI wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Naghenjwa Kaboyoka, amekalia kuti kavu kutokana na kutoa taarifa za kamati hiyo kwa vyombo vya habari kabla hazijaidhinishwa na Spika, kinyume cha Kanuni za Kudumu za Bunge Toleo la Januari 2016.

MWENYEKITI wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Naghenjwa Kaboyoka.

Kaboyoka (68), ambaye pia ni Mbunge wa Same Mashariki na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), alinukuliwa na moja ya vituo vya televisheni nchini juzi akieleza mahojiano yaliyofanywa na kamati yake dhidi vigogo wa Benki Kuu (BoT), Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) na Mbunge wa Ulanga, Goodluck Mlinga (CCM).

Vigogo hao akiwamo Gavana wa BoT, Prof. Florence Luoga, walifikishwa mbele ya kamati hiyo wiki iliyopita baada ya Mlinga kudai BoT hutumia Sh. bilioni 12 kwa mwaka kugharamia ughaibuni matibabu ya watumishi wake.

Kutokana na uzito wa tuhuma hizo, Spika wa Bunge, Job Ndugai aliiagiza PAC inayoongozwa na Kaboyoka kufuatilia ukweli wa madai hayo kwa kuwahoji Mlinga, NHIF pamoja na bodi na menejimeti ya BoT na kumpatia taarifa kufikia juzi.

Hata hivyo, muda mfupi baada ya kamati hiyo kukabidhi ripoti yake kwa Spika, Kaboyoka alinukuliwa na moja ya vituo vya televisheni akizungumzia suala hilo kabla ya ripoti kuidhinishwa na Spika, kitendo kilichodaiwa na Mlinga kuwa ni kinyume cha Kanuni za Bunge.

Mara tu baada ya kumalizika kwa kipindi cha 'Maswali' bungeni jijini hapa jana asubuhi, mbunge huyo alisimama na kuomba mwongozo wa Kiti cha Spika cha Spika kuhusu suala hilo.

"Mheshimiwa Mwenyekiti, kamati zetu zinapoagizwa na Spika zifanye kazi, zinatakiwa zipeleke ripoti kwa spika ndipo aitolee ufafanuzi," Mlinga alisema na kueleza zaidi:

"Mwisho wa wiki niliongea kuhusu BoT kutumia fedha nyingi kwa ajili ya matibabu kuliko taasisi nyingine za serikali ambazo zinafanya kazi ngumu.

"Mheshimiwa Mwenyekiti kamati ya PAC ilikaa na mimi, NHIF na BoT. Taarifa nilizokuwa nazo hadi sasa bado Spika hajalitolea majibu suala hilo.

"Lakini jana (juzi) niliona kwenye taarifa ya habari Mwenyekiti wa PAC akitoa taarifa ya kamati ambayo ni siri mpaka Spika atakapotolea majibu, akisema taarifa kuhusu BoT kutumia fedha nyingi kwenye matibabu si za kweli.

"Mheshimiwa mwenyekiti, naomba kupatiwa utaratibu kama na mimi naweza kulizungumzia suala hilo kwenye vyombo vya habari kwani hata mimi nilizongwazongwa na vyombo vya habari lakini niliheshimu kanuni.

"Naomba nipatiwe utaratibu kwani hata mimi naweza kuzungumza na nikizungumza kuna watu watakimbia ofisi zao."

Katika majibu yake kwa mbunge huyo, Mwenyekiti wa Bunge, Najma Murtaza Giga aliyekuwa anaongoza kikao cha jana cha Bunge, alisema kilichofanyika ni kinyume cha Kanuni za Bunge na Spika atalishughulikia.

Giga pia alimtaka Mlinga kutolizungumza suala hilo kwenye vyombo vya habari kwa kuwa kufanya hivyo ni ukiukaji wa kanuni za chombo hicho cha kutunga sheria.

Tuhuma za BoT kutumia mabilioni ya shilingi kugharamia matibabu ya ughaibuni ya maofisa wake ziliibuliwa na Mlinga bungeni Jumatatu ya wiki iliyopita wakati wa mjadala wa makadirio ya bajeti ya Wizara ya Fedha na Mipango kwa mwaka ujao wa fedha.

Mbunge huyo alidai: "BoT ndiyo inayotumia fedha nyingi kuliko taasisi yoyote. Ukiumwa mafua unakwenda Uingereza. Matumizi yao yamepanda kutoka Sh. bilioni moja na sasa wanatumia Sh. bilioni 12 kwa sababu watu wana maslahi binafsi.

“Wanasema wao hawawezi kwenda NHIF kutibiwa kwenye hospitali za ndani. Kuna ufisadi mkubwa BoT. Siungi mkono hoja ya Waziri (wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango) hadi akija na majibu ya haya.”

Habari Kubwa